Thursday 26 December 2013

Na Mohamed Said

HISTORIA ya TANU ingelipotea kabisa kama siyo juhudi za makusudi za Profesa John Illife wa Cambridge aliyekuwa mwalimu wa historia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika miaka ya katikati ya 1960.

Illife alipogundua tatizo lililokuwapo katika historia ya uhuru wa Tanganyika na hasa historia ya TANU na nafasi ya Julius Nyerere katika kuanzishwa kwake alifanya azma ya kuitafiti na kuiandika. John Illife aliwaagiza wanafunzi wake kutafiti na kuandika maisha ya wazalendo waliofanya mambo ya kutukuka katika sehemu zao. Zoezi hili lilipokamilika palipatikana historia za wazalendo wengi na kazi hii ikazaa kitabu “Modern Tanzanians” ambacho Iliffe alikihariri na yeye mwenyewe akiwa mmoja wa watu waliochangia uandishi akaandika maisha ya Martin Kayamba.

Kitabu hiki kina habari za maisha ya Watanganyika 12 ambao waliishi miaka ya mwanzo ya karne ya ishirini wakati wa utawala wa Wajerumani hadi kufika kwa Waingereza. Katika kitabu hiki kitu kimoja kinachojitokeza dhahiri ni kuwa wazalendo wote walioshiriki katika kutafuta Uhuru wa Tanganyika walikuwa Waislam. (Kleist Sykes, Ali Ponda na Hassan Suleiman) wao maisha yao yalijikita katika siasa za ukombozi wa Tanganyika kutoka ukoloni wa Waingereza wakati wenziwao Wakristo Canon Kolumba Msigala, Pastor Yohane Nyagava na Bishop Jeremiah Kissula) historia ya maisha yao ilikuwa katika nyanja za utumishi wa kanisa.

Hali hii imeendelea hadi ilipofika wakati wa kuasisiwa kwa TANU. Katika ukweli huu ndipo palipo tatizo la wanahistoria kuiogopa historia ya kweli ya TANU kwa kuwa harakati zilichukua mkondo mkali wa Waislam kupinga ukoloni kwa dhati. Kwa ajili hii basi historia nzima ya kudai uhuru imejaa majina ya Waislam. Hili ni moja ya sababu inayofanya historia hii iwe nyeti, iogopewe na isitafitiwe na kuandikwa inavyopaswa. Hili ni tatizo la kwanza.

Tatizo la pili ni watafiti kwa hofu au kwa kutaka kujipendekeza kwa Mwalimu Julius Nyerere kupuuza michango ya wale waliokuwa katika harakati za kupambana na ukoloni ama kabla ya Nyerere au walikuwa pamoja nae. Watafiti hawa pamoja na hata wanasiasa ndani ya TANU kwa wakati ule wakawa wanashindana katika kumjazia sifa Mwalimu Nyerere kuwa kwa hakika kabla yake hapakuwa na harakati zozote za kutaka kuikomboa Tanganyika. Hali hii iliendelea kwa kipindi kirefu hadi kwa mara ya kwanza mmoja kati ya waasisi wa TANU, marehemu Joseph Kasella Bantu alipoandika kueleza mchango wake katika kuunda TANU.

Katika makala ile Kasella Bantu alijigamba kwa kusema kuwa yeye ndiye aliyeitisha mkutano mkuu wa mwaka 1954(New African March 1985). Kassela Bantu ikawa hapa kama vile kafungua sanduku la Pandora kwa kuwa palitokea watu wakampinga kuwa hakusema kweli yote katika nukta ile. Mwandishi wa makala hii akiwa mmojawapo alimpinga Kassela Bantu (New African May 1985) kwa kusema kuwa kama ipo haja ya kutoa sifa kwa mtu mmoja mmoja basi sifa ile alistahili zaidi marehemu Abdulwahid Sykes. Mchango wa familia ya Sykes katika kuiasisi African Association na baadae TANU umejipembua vyema na unafahamika. Huu ndio ukweli wa historia ya TANU na mambo yalivyokuwa kati ya mwaka 1929 ilipoasisiwa African Association (AA) hadi 1954 TANU ilipozaliwa, iwe wanahistoria wanatambua au vinginevyo.

Sasa kwa kujua au kutojua Mwalimu Nyerere ambae maisha yake yote hakupenda kuizungumzia historia ya TANU au habari za wazalendo waliokuwapo katika siasa kabla yake, katika kuadhimisha miaka 30 ya Azimio la Busara mjini Tabora Mwalimu Nyerere alitoa hotuba kuhusu umuhimu wa kuwatambua wazalendo walioijenga TANU kati ya mwaka 1954 - 1958. Sababu ya kusema maneno hayo lilikuwa swali aliloulizwa katika mkutano wa hadhara na Mzee Ramadhani Singo mmoja wa wanachama shupavu wa TANU Tabora. Singo alimkabili Mwalimu Nyerere na kumuuliza ‘Mwalimu mbona umetusahau wenzako?’ Swali lile liligusa hisia za Mwalimu na ile hadhira iliyokuwapo pale. Ndiyo katika kujibu swali lile Mwalimu Nyerere akawaadhimisha mashujaa walioingia TANU zile siku za mwanzo.

Kikundi kile cha wapigania uhuru wa TANU waliokuwa pale mkutanoni mbele ya Mwalimu takriban wote walikuwa wazee katika kanzu mbovu na nguo zilizochakaa. Katika hali ile hawakutoa picha iliyompendeza yeyote. Mwalimu Nyerere akiwa hakika katahayari kwa kuwaona wapigania uhuru wenzake walivyokuwa taabani aliona ipo haja kwa wakati na saa ile kuwaadhimisha. Ndipo aliposema waasisi wa TANU waheshimiwe. Sasa basi kwa Mwalimu Nyerere tokeo kama hili lilikuwa la pili kumtokea. Hali kama ile ilimtokea Kizota alipokutana na Dossa Aziz.

Mwaka 1987 katika Mkutano maarufu wa Kizota ndipo Nyerere alikutana na Dossa Aziz uso kwa uso baada ya miaka mingi kupita. Dossa mfadhili mkubwa wa Mwalimu na TANU alikuwa kachoka kwa shida. Dossa sasa alikuwa masikini na hali yake haikuweza kujificha. Kila aliyemjua Dossa na enzi zake alishtushwa na hali yake. Inasemekana hata nguo za kuvaa kuja katika mkutano wa Kizota ilibidi anunuliwe na rafiki yake mpenzi toka utotoni waliosoma darasa moja hapo Shule ya Kichwele (sasa Shule ya Uhuru) Balozi Abbas Sykes. Dossa aliweka mfuko wake wazi kwa Nyerere na TANU katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Kadi yake ya TANU ni namba 4. Dossa ndiye aliipa TANU gari yake ya kwanza – Land Rover ambayo ndiyo iliyomtembeza Nyerere nchi nzima wakati wa kuitangaza TANU kwa wananchi.

Waliomjua Dossa na ukarimu wake walilia kwa kwikwi wakati wa mazishi yake. Waliona uchungu kwa kuwa Dossa hakuwa mtu wa kupanga foleni kungoja tiba Hospitali ya Tumbi. Hali ya Dossa ilimgusa sana Mwalimu Nyerere na haikupita muda Mwalimu alimnunulia Dossa gari imsaidie.

Turudi kwa Baba wa Taifa. Sasa kwa mara ya pili katika kipindi kisichozidi mwaka hali kama ile ya Dossa aliyoiona Kizota alikuwa anaiona tena kwa wazee wa Tabora – wapigania uhuru wa Tanganyika waliochoka na kupigwa sawasawa na ufukara. Ilikuwa lazima Mwalimu aseme kitu kuhusu hawa wazalendo aliowasahau au waliosahauliwa na historia na wakati. Mwalimu kwa kuwatukuza waasisi wale alisema kuwa siku za mwanzo za TANU zilikuwa ngumu na chama lazima kiwaheshimu wale wanachama wa mwanzo. Kwa kauli ile Mwalimu Nyerere akawa kanifungulia mimi njia ya kupita kwa kuunga mkono maneno yake. Nikaandika makala ambayo kwa mara ya kwanza nikasema kuwa historia ya TANU haiwezi kukamilika bila kutaja mchango wa Waislam na bila ya kumtaja Abdulwahid na Ally Sykes, Saadani Abdu Kandoro, John Rupia na Dossa Aziz (In Praise of Ancestors: Africa Events March/April 1988).

Mwalimu alichukua uongozi wa TAA toka kwa Abdulwahid Sykes. Uchaguzi huu una kisa kirefu cha kusisimua wakati mwalimu wa shule asiyejulikana Julius Nyerere kutoka Musoma alipomuangusha kwa kura chache sana ndani ya Ukumbi wa Arnatouglou Abdulwahid Sykes, kijana maarufu wa mjini na mtoto wa mmoja wa waasisi wa African Association ambaye baba yake, Kleist Sykes alifanya mengi katika maendeleo ya Waafrika kati ya vita kuu mbili za dunia. Inasikitisha sana kuona kuwa kipande hiki cha kupokezana uongozi kati ya marehemu Abdulwahid Sykes na Nyerere ni katika historia inayofanywa nyeti.
Wanasiasa wetu na hata Nyerere mwenyewe katika umri wake wote wa siasa aliijenga fikra yake vyema kiasi kuwa alifanikiwa kufuta katika ubongo wake ni vipi alikuja kupata uongozi wa TAA. Katika maisha yake yote hakupata hata siku moja kutamka majina ya wazalendo wenzake aliokuwa nao kati ya mwaka 1953 hadi 1961 Tanganyika ilipojikomboa.

Katika kupuuza historia ya siasa kabla ya kuja kwa Mwalimu Nyerere viongozi wetu imewalazimu kubadilisha msamiati. TAA chama ambacho kilidumu kwa miongo miwili kikipigania haki ya Mwafrika kikawa baada ya kuundwa TANU kinakejeliwa na wanasiasa wapya na watafiti wa historia ya uhuru wa Tanganyika. Ikawa kila inapotajwa TAA ile sura yake ya chama cha siasa huvuliwa kikaitwa ‘chama cha starehe.’ Kwa maana ya kuwa TAA haikuwa lolote hadi Nyerere alipofika na wasemavyo wenyewe kuanzisha TANU.

Kwa mantiki hii ikawa lazima ilazimishwe kuwa TANU iliasisiwa na Mwalimu Nyerere peke yake bila ya msaada wa yeyote. Huu ndio ukawa mwelekeo hata wa Mwalimu Nyerere. Historia yote ya nyuma hadi kufikia mwaka 1954 ilipoundwa TANU ikazikwa na ikawa kama vile ni usaliti kuwataja wazalendo wengine waliokuwa katika siasa kabla ya Mwalimu Nyerere.

Leo hii wangapi wanajua kuwa siku ya mwisho walipokubaliana kuunda TANU mkutano huo ulifanyika Makao Makuu ya TAA New Street kwenye chumba kidogo kilichukuwa na samani duni? Ndani ya chumba kile walikuwapo wanakamati ya ndani ya TAA - Abdulwahid, Ally, Dossa, Mzee Rupia na Nyerere. Baadhi yao katika chumba kile walikuwa wamepindua masanduku ya bia na kuyakalia kwa kuwa viti vilikuwa havitoshi. Vyumba katika ofisi ile ya TAA vilikuwa vimepangishwa Muhindi aliyekuwa akifanya kazi ya kufua nguo (dobi).

Hiyo ndiyo siku walipokubaliana kuwa hapana sababu tena ya kusubiri. Wakati wa kupiga mbiu ya mgambo kuanzishwa TANU umefika. Baada ya uamuzi huu kufanyika Dar es Salaam, mjini Tabora Salum Abdallah na wazalendo wengine mmojawapo akiwa marehemu Abubakar Mwilima, George Magembe na wengine walikutana kwa siri kupanga mipango ya kumsafirisha Germano Pacha aliyekuwa katibu wa TAA Western Province kuja Dar es Salaam kuhudhuria mkutano wa kuanzishwa kwa TANU Julai 7 1954.

Salum Abdallah hatajiki popote katika historia ya TANU lakini ana kisa cha kusisimua katika maisha yake ya siasa kuanzia mwaka 1947 hadi alipowekwa kizuizini mwaka 1964 akiwa Mwenyekiti wa Tanganyika Railway Africa Union (TRAU). Salum Abdallah amekufa akiwa ameacha nyuma hazina kubwa ya kumbukumbu ya harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Vipi leo tuambiwe bila hata ya chembe ya aibu ati African Association iliyokuja kubadilishwa jina na kuitwa Tanganyika African Association kilikuwa chama cha starehe?

Historia ya TANU yenyewe inakataa hili achilia mbali historia ya mzalendo mmoja mmoja na michango yao katika kudai uhuru. Kumbukumbu hizi zina uwezo wa kumsisimua mtafiti yeyote. Inasikitisha na kutia hofu kuwa nyaraka nyingi za TANU na nyingine zinazomuhusu Mwalimu Nyerere na uhuru wa Tanganyika kumbukumbu ambazo ni muhimu kwa historia ya nchi hii ziko mikononi mwa watu binafsi na nyingine hazitopatikana kabisa.

Mathalan wangapi leo wanajua habari za Erika Fiah au Ramadhani Mashado Plantan. Hawa ndio wazalendo wa mwanzo kufungua magazeti yaliyokuwa sauti ya Waafrika. Fiah alikuwa mmoja wa wanasiasa wa mwanzo kabisa wa mrengo wa kushoto na kalamu yake katika gazeti lake Kwetu alilolianzisha mwaka 1937 ilikuwa ikitema cheche kali dhidi ya ukoloni.

Nani anajua kuwa gazeti la kwanza kumpa Mwalimu sauti na kueneza sera za TANU lilikuwa Zuhra mhariri akiwa Plantan? Makala za Fiah katika gazeti lake la Kwetu ingawa zimeandikwa zaidi ya nusu karne sasa bado zina msisimko kwa msomaji kama vile kaziandika jana.

Au nani leo anamjua Mzee Yusuf Olotu maarufu Yusuf Ngozi wa Moshi na jitihada zake za kuipa TANU ushindi wa kishindo katika Uchaguzi wa Kura Tatu mjini Moshi. Au mchango wa Sheikh Yusuf Badi wa Lindi au mchango wa Dk Michael Lugazia, Dk Luciano Tsere, Dk Joseph Mutahangarwa, Dk Vedasto Kyaruzi, Dk Wilbard Mwanjisi na wengineo?

Kwa kuhitimisha, haya niliyoandika ni mifano michache tu katika dondoo za historia ya nchi yetu. Naamini wapo wazalendo wengi huko mikoani ambao kwa njia moja au nyingine wamefanya mengi katika historia ya   uhuru wa Tanganyika. Kizazi kilichopo sasa kina wajibu mkubwa wa kutafiti habari zao, kuzihifadhi na kuwapa heshima wanayostahili.

Alipokufa Dossa Aziz ilipofika wakati wa CCM kutoa rambirambi zao hawakujua waseme nini kwa kuwa viongozi waliokuwapo hakuna hata mmoja aliyekuwa anajua mchango gani Dossa alitoa kwa Nyerere na TANU na kwa bahati mbaya sana Mwalimu Nyerere hakuhudhuria mazishi yale.

Juma Volter Mwapachu katika tanzia aliyomwandikia Dossa, ‘Dossa Aziz a Fallen Hero’ (The African 12 May 1998) alimlaumu Mwalimu kwa kukaa kimya kuhusu wapigania uhuru wenzake kiasi kuwa hakuna chochote kinachojulikana kuhusu mchango wao.

Hali hii ilijitokeza pia katika mazishi ya Mzee Paul Bomani hakuelezwa kama ilivyostahili. Kwanini tuogope kuieleza historia vilivyo?

0 comments:

Post a Comment

99Graphix

99Graphix
99Graphix
Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!