Mohamed
Said
Nimesoma makala
kuhusu Mzee Lameck Makaranga Bogohe (Nipashe Julai 7, 2010) iliyoandikwa na
Denis Maringo ambae ametambilishwa kama Mwanahistoria na Mwanasheria kitaaluma
na ni Mkurugenzi wa Kituo cha Haki na Demokrasia - Centre for Justice and
Democracy (CJD).
Inaelekea nia ya makala hiyo ilikuwa
kuwakumbusha wananchi historia ya kuasisiwa kwa TANU na waasisi wake hasa kwa kuwa
tulikuwa katika sikukuu ya saba saba ambapo tunakumbuka siku TANU chama
kilichopigania uhuru wa Tanganyika kilipoanzishwa tarehe 7 Julai 1954. Ajabu ni
kuwa katika vitu vinavyostaajabisha sana ni kupuuzwa kwa historia hii
iliyotukuka ya kudai uhuru wa Tanganyika pamoja na kupuuzwa kwa wazalendo
walijitolea muhanga wakati ule kuhakikisha kuwa Tanganyika inajikwamua kutoka
katika makucha ya ukoloni wa Waingereza. Mzee Bogohe analalamika kwa kusema
kuwa “…katika vitabu kila Tanu iandikwapo ni Mwalimu Nyerere.” Kwa hakika Mzee
Bogohe si wa kwanza kuliona hili hata mie kuna wakati hili jambo lilikuwa
likinistaajabisha sana hata nikafikia kuona kuwa labda CCM chama kilichokuja
baada ya TANU hawajipendi na hawawapendi mashujaa wao lakini nikajagundua kuwa
si kama hawajipendi ila hawapendi historia ya wazalendo wengine wanapenda
historia ya Julius Nyerere peke yake na atajwe pweke bila ya kumuhusisha na
yeyote yule.
Mzee Bogohe amesema mengi kuhusu
udhaifu huu lakini mie sitanukuu moja baada ya jingine katika masikitiko yake
ila nitazungumza kwa ujumla tu na kujaribu kusahihisha yale ambayo nimeona
labda kwa uzee, siku kuwa nyingi kupita na kwa kukosa nyaraka halisi za rejea
za historia ya kuanzishwa kwa TANU kuna mengi mzee wetu ameyasahau au ameyakosea
kwa tarehe na maudhui yenyewe katika matokeo yaliyopelekea kuundwa kwa African
Association mwaka 1929 na katika kuigeuza African Association kuwa Tanganyika
African Association (TAA) mwaka 1948 na mwishowe kuundwa kwa TANU 1954. Katika
maelezo hayo nitaelezea vilevile harakati zilizokuwapo pale New Street Makao
Makuu ya TAA wakati wazalendo viongozi wa TAA kati ya 1950 – 1953 walipokuwa
wanapanga mikakati ya kuunda TANU. Wakati huo ni ukweli usiopingika kuwa hakuna
kati yao ukimtoa Hamza Mwapachu na Joseph Kasella Bantu aliyekuwa amemsikia
Julius Nyerere.
Imethibitika hivi sasa kuwa Nyerere
hakupendezewa na historia ya kweli ya kudai uhuru wa Tanganyika ambayo ilianza miaka
mingi nyuma kabla yake kiasi cha takriban nusu karne. Historia ya African Association
(baadae chama kikaja kujulikana kama Tanganyika African Association - TAA)
chama kilichokuja kuunda TANU 1954 inaanza katikati ya miaka ya 1920 na kinara
wa harakati hizo alikuwa Kleist Sykes (1894 - 1949) baba yao marehemu
Abdulwahid (1924 – 1968), Ally na Abbas Sykes.
Kumbukumbu za Kleist zinaonyesha kuwa alitiwa hamasa za kuanzisha
African Association na Dr Dr James Kwegyir Aggrey kutoka Ghana aliyekuja
kutembelea Tanganyika mwaka wa 1924. Kleist alikuwa Mwafrika msomi katika
kiwango cha enzi zile akizungumza Kiingereza na Kijerumani. Dr Aggrey katika
mazungumzo na viongozi wa Dar es Salaam Waafrika akiwamo Kleist Sykes aliwashauri
viongozi wale kuwa ili kupata maendeleo haraka itakuwa busara kwa wao kama
Waafrika kuwa na chama chao kitakachowajumuisha Waafrika wote. Ilimchukua
Kleist na wenzake miaka mitano hadi kufikia kusajili African Association mwaka
1929 Kleist akiwa katibu mwanzilishi na Mzee Bin Sudi akiwa rais wake. Viongozi
hawa baada ya kuasisi African Association wakaasisi chama kingine Al Jamiatul
Islamiyya fi Tanganyika mwaka 1933. Mingi ya mikutano ya kuanzisha African
Association ikifanyika nyumba moja Mtaa wa Magila Mission Quarters, nyumba hii
baadae ilikujanunuliwa na John Rupia. Hii nyumba bado ipo hadi leo.
Wanahistoria bado wananafasi ya kwenda izuru nyumba hii kabla haijavunjwa na
kujengwa ghorofa.
Historia ya TANU ukiitaka kwa undani
inaanza miaka hii 1929 na mwanzoni mwa
1930. Sasa kupitia vyama hivi viwili viongozi wake wakajenga majengo
mawili, moja ni hiyo nyumba ambayo hadi leo ipo ambayo yalikuwa makao makuu ya
African Association Mtaa wa New Street. Jengo hili lipo na lilikuja kufunguliwa
na Gavana Ronald Cameroon mwaka 1933. Bwana Ally Sykes ana picha ambayo inaonyesha
sherehe za ufunguzi wa jengo hilo ikimwonyesha baba yake, Gavana Cameroon,
Mwalimu Mdachi Shariffu, Machado Plantan na viongozi wengine wa African
Association. Hii ndiyo nyumba iliyokuja kuasisiwa TANU mwaka 1954. Marehemu
Abdulwahid Sykes katika kumbukumbu zake anasema yeye alikuwa akifuatana na baba
yake kila siku za Jumapili pale New Street na akimuona baba yake na viongozi
wenzake wakijenga nyumba ile kwa kujitolea. Jengo la pili ni hilo ambalo sasa
ni shule ya Msingi ya Lumumba ambapo zamani ilikuwa makao makuu ya Al Jamiatuli
Islamiyya na vilevile ilikuwa Al Jamiatul Islamiyya Muslim School. Viongozi wa
mwanzao na wanachama wa awali wa TANU walitokana na vyama hivyo viwili. Taarifa
hizo zote na kumbukumbu nyingine za harakati za siasa katika Tanganyika zipo
mpaka leo katika hifadhi ya familia ya akina Sykes. Mwandishi wa makala hii
zilimsaidia sana katika kuandika kitabu, The
Life and Times of Abdulwahid Sykes 1924 -1968 The Untold Story of the Muslim
Struggle Against British Colonialism in Tanganyika kitabu kilichochapwa
London mwaka 1998 na tafasiri yake ya Kiswahili kuchapwa na Phoenix Publishers,
Nairobi mwaka wa 2002.
Historia hii ya TANU kama ilivyo hapo
juu ilikuja kuandikwa na Abdulwahid Sykes na Dr Wilbert Kleruu mwanzoni mwa
miaka ya 1960 kwa ushauri wa Mwalimu Nyerere, Mwalimu Kihere na Dossa Aziz. Inasemekana
historia ile kama alivyokuwa akiandika marehemu Abdulwahid Sykes ikawa kama
inamtia unyonge kidogo Nyerere. Nyerere hakuipenda historia ile. Kwa
hakika historia hii ambayo yeye hayumo hakuipenda kabisa na ikabidi mradi huo
wa kuandika historia hiyo ufe kabla ya kazi kukamilika. Abdulwahid Sykes
akajitoa katika kazi hiyo akamuuacha Dr Kleruu yeye aendeleenayo. Kleruu
alimaliza kazi hiyo kwa namna inavyosemekana alivyoelekezwa na Nyerere lakini
mswada ukabaki pale Makao Makuu ya TANU bila kuchapwa kwa muda mrefu. Inasemekana
mswada uliibiwa na ukajachapwa kitabu bila ya ridhaa ya TANU. Hata hivyo haijulikani
nyaraka zile za mwanzo kama zilivyoandikwa na Abdulwahid Sykes ziko wapi
kwa sasa kwani juhudi za mwandishi
kuzipata katika maktaba ya CCM Dodoma ziligonga mwamba.
Baada ya wizi
huo TANU ikaunda jopo la wataalamu wake ambalo lilikaa kitako na kuandika
historia ya TANU na kitabu kikachapwa (Historia ya Chama Cha TANU 1954-1977,
Dar es Salaam, Kivukoni Ideological College, 1981). Kitabu hiki kilipotoka
wengi hasa sie wazaliwa wa Dar es Salaam kikatustaajabisha kwani kwa kweli
kilikuwa kitu kingine, ile haikuwa historia ya TANU na haitakujakuwa. Kwa
uchache unaweza kusema ilikuwa historia yake Nyerere kuanzia mwaka wa 1954 na
hata hivyo ilikuwa ikichagua nini la kuandika jina gani la kutaja na lipi la
kukwepa. Kwa nini nasema kukwepa? Kitabu kizima hakuna hata sehemu moja ambako
waasisi wa siasa za Tanganyika - ukoo wa akina Sykes ulipotajwa. Huwezi kuandika
historia ya Nyerere ukaacha kuwataja watu hawa na wazalendo wa Dar es Salaam
waliomtia katika siasa za TAA na TANU watu kama Mwinjuma Mwinyikambi, Jumbe
Tambaza, Mshume Kiyate, Iddi Tosiri na ndugu yake Iddi Faizi na kaka yao Sheikh
Mohamed Ramia wa Bagamoyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Suleiman
Takadir, Dossa Aziz, Hamza Mwapachu, Clement Mtamila, Dr Michael Lugazia, John
Rupia, Dr Vedasto Kyaruzi, Dr Luciano Tsere,
Dome Budohi, Dennis Phombeah, Zuberi Mtemvu, Ali Mwinyi Tambwe, Tatu binti
Mzee, Titi Mohamed, Asha Ngoma na majina kwa kweli ni mengi ukisema uyataje
hutoweza kuyamaliza kwa ukamilifu wake. (Titi Mohamed amehutubia mkutano wa
TANU miezi michache baada ya kuundwa kwa TANU pale Mnazi Mmoja hamjui Nyerere
wala hajaona sura yake inafananaje). Ikawa sasa historia hii ya ukwepaji baadhi ya
majina ya wazalendo Mwalimu akaipenda na ndiyo ikawa historia rasmi inayokubalika
ya TANU na harakati za kudai uhuru hadi leo.
Katika hali kama
hii ndipo ikawa watu kama Mzee Bogohe lau kama walikuwa na mchango wao katika
siasa za kudai uhuru wa Tanganyika wakawa wamewekwa pembeni hawatajwi anatajwa
Nyerere peke yake. Itoshe kumaliza kipengele hiki kwa kusema kuwa katika
chaguzi za siasa za kusisimua katika historia ya Tanganyika ni ule uchaguzi wa
TAA wa 1953 wakati Nyerere alipogombea nafasi ya urais wa TAA dhidi ya rais
wake aliyekuwa anamaliza kipindi chake Abdulwahid Sykes pale katika ukumbi wa
Arnatouglo tarehe 17 April 1953. Kukutana kwa Abdulwahid Sykes na Nyerere mwaka
wa 1952 na siri za harakati alizozikuta Nyerere kwa Abdulwahid Sykes ni kisa
cha kumsisimua mtafiti yeyote wa historia. Mama Maria Nyerere lazima atakuwa na
kumbukumbu hizi za wao na akina Sykes pale mtaa wa Kipata nyumbani kwa Ally
Sykes na Aggrey Street nyumbani kwa Abdulwahid Sykes na pilka pilika za hatari za
kuwakwepa makachero wa Special Branch wakiongozwa na Amri Kweyamba na vijana
wake. (Amri Kweyamba alidumu katika kazi hiyo hata baada ya uhuru lakini sasa
akiitumikia serikali ya TANU na Nyerere siyo ile ya Gavana Edward Twining). Pale
Kipata ndipo Ally Sykes alipokuwa ameficha mashine ya kudurufu ambayo alikuwa akichapa makala za siri
(Waingereza wakiziita za uchochezi) kuhamasisha Waafrika dhidi ya ukoloni. Shajara
za Abdulwahid Sykes za kipindi hiki (1950 - 1954) ameziandika kwa hati mkato na
inasikitisha kuwa hadi leo akina Sykes hawajataka kuzitoa kwa watafiti zisomwe
kwa faida ya historia ya nchi yetu na kizazi kijacho.
Wazee wengi wa
Dar es Salaam na wengi wao weshatangulia mbele ya haki wanafahamu fika kuwa
kama unataka kumpa sifa mtu mmoja kwa kuanzisha TANU basi hatakuwa Nyerere sifa
hiyo ni ya marehemu Abdulwahid Sykes ambae katika uongozi wake kuanzia 1950
hadi 1953 ndipo aliposhughulikia katiba ya TANU na kuleta mbinu mpya ya
kupambana na Waingereza kiasi cha kuwa baada ya majalada ya Kiingereza kule
London kuwekwa wazi (baada ya kupita miaka 50) taarifa za siri za kikachero za
Special Branch zinaonyesha kuwa Abdulwahid walimchukulia kama mtu ”hatari.”
Alikuwa hatari kwa kuwa ndani ya TAA katika miaka ya mwanzo ya 1950 Abdulwahid
akiwa ndiye rais TAA ilikuwa na uhusiano na harakati za Mau Mau chini ya akina
Kenyatta na Bildad Kaggia huko Kenya na Kenneth Kaunda toka Northern Rhodesia.
Itoshe tu kusema mwaka 1950 Abdulwahid Sykes alifanya mkutano wa siri na
viongozi wa KAU Nairobi wakiwemo Kenyatta mwenyewe, Kaggia, Kungu Karumba na
wengine nia ikiwa ni kuunganisha nguvu za Tanganyika na Kenya katika kuupiga
vita ukoloni. Kisa cha Ally Sykes na Kenneth Kaunda ni kisa kingine cha
kusisimua sana. Baada ya kuwasiliana na Kaunda mwaka 1953 na Kaunda kumwalika
Ally Sykes na Dennis Phombeah katika mkutano wa wanaharakati wa ukombozi kusini
ya Afrika uliokuwa ufanyike Lusaka Ally Sykes na Dennis Phombeah waliishia mbaroni
mjini Salisbury Southern Rhodesia. Hizi ndizo zilikuwa harakati za TAA pale
Makao Makuu na hawa ndiyo walikuwa viongozi walokuja iasisi TANU.
Niongeze kidogo
kwa kusema kuwa na hili suala la katiba ya TANU wala si kitu cha kukipigia sana
kelele kwani walichofanya viongozi wa TAA ilikuwa kunakili katiba ya Convention
Peoples Party (CPP) chama alichokianzisha Kwame Nkrumah. Mahali palipoandikwa
CPP viongozi wa TAA waliweka TANU. Kwa hakika kama kuna kitu cha kujivunia
katika maandiko yaliowahi kuandikwa na TAA basi ni ile memorandum ya TAA Political
Subcommittee iliyotayarishwa mwaka 1950 na uongozi wa TAA na kusainiwa na
viongozi hawa wafuatao: Abdulwahid Sykes, Sheikh Hassan bin Amir kama Mufti wa
Tanganyika na Zanzibar; Dr Vedasto Kyaruzi, Hamza Mwapachu, Said
Chaurembo, John Rupia na Stephen Mhando.
Waraka huu ndiyo Nyerere alikwendanao Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwaka wa
1955 na kuusoma mbele ya Baraza la Udhamini. Hiki ndicho kitu cha kuringia na
kujivunia si hiyo katiba ya TANU waliyonyambua toka kwa Nkrumah. Inasemekana
hatima iliyoikumba ile kazi ya historia iliyoandikwa na Abdulwahid Sykes
kuibiwa pale Makao Makuu ya TANU imeikumba na nyaraka hii muhimu ya kihistoria
iliyotayarishwa mwaka 1950 na viongozi wa TAA. Haishangazi leo ukisikia baadhi
ya viongozi wakiikashifu TAA wakinadi kinywa kipana na bila ya soni ati TAA
hakikuwa chama cha siasa bali kilikuwa chama cha starehe.
Mzee Bogohe
anasema jina la TANU kalitoa yeye na anataka atambulike kwa hilo, sawa. Wangapi
leo wanajua kuwa kadi za TANU za kwanza 1000 alizitengeneza Ally Sykes na
akazilipia kutoka mfukoni kwake binafsi? Wangapi leo wanajua kuwa kadi ya
Nyerere ya TANU ni namba 1 na imetiwa saini na Ally Sykes? Wangapi wanajua kadi
namba 2 ya TANU ni ya Ally Sykes
mwenyewe na namba 3 ni ya kaka yake Abdulwahid Sykes? Vipi kaka mtu apate kadi
namba 3 na mdogo namba 2 ikiwa utamaduni wa Kiafirika na adabu zetu ni
kumtanguliza mkubwa mbele? Majibu yapo na ndiyo yanayokoleza utamu wa historia
ya kweli ya TANU. Kinyume cha hapo utapambana na historia ya kubuni na kitu cha
kubuni au kisichokuwa na ithibati siku zote huwezi kukitegemea kujenga hoja
thabiti.
Hapa si mahali
pale kuyaeleza yote hayo. Bwana Ally Sykes yu hai na wanahistoria waende
wakamhoji watapata faida kubwa. Sasa na tujiulize, lipi kubwa. Kutoa jina la
TANU au kukianzisha chama chenyewe cha TANU? Historia imeshuhudia kuwa hadi
anaingia kaburini marehemu Abdulwahid Sykes hakupata kukumbusha kuwa TANU chanzo
chake ni baba yake au kuwa yeye ndiye aliyemweka Nyerere katika uongozi wa TAA
na mwishowe TANU. Msisitizo ni kuwa hadi marehemu Abdulwahid Sykes anaingia kaburini
1968 hakupata kujinasibu kwa kuanzisha TANU wala kusema kuwa alikuwa yeye ndiye
aliyempa Nyerere nafasi ya uongozi kwanza katika TAA 1953 na kisha 1954 katika
TANU. Abdulwahid Sykes kwa waliomjua wanasena alikuwa mtu muungwana sana. Juu
ya hayo yote alofanya ukiondoa kuwa alikuwa kati ya wafadhili wanne wa awali wa
TANU wengineo wakiwa mdogo wake, Ally, John Rupia na Dossa Aziz hawa wote
wametolewa katika kumbukumbu za historia ya TANU. Ukikisoma kitabu cha historia
ya TANU kilichoandikwa na Kivukoni College hili utaliona dhahiri.
Tumalize kisa
chetu. Yapo makosa kidogo katika simulizi ya Mzee Bogohe bila shaka ni kwa
sababu ya miaka mingi kupita. Mzee Bogohe anasema kuwa Mhasibu Mkuu wa kwanza
wa TANU alikuwa Julius Mwasanyangi. Ukweli ni kuwa mweka hazina wa kwanza wa
TANU alikuwa Iddi Faizi Mafongo aliyekuwa mhasibu vilevile wa Al Jamiatul
Islamiyya. Iddi Faizi Mafongo ndiye aliyekuwa na jukumu la kukusanya fedha za
safari ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa mwezi Machi 1955. Katika nafasi yake
ya kuwa mweka hazina wa vyama hivyo viwili Iddi Faizi alitoa fedha katika
hazina ya za Al Jamiatul Islamiyya na kuzitia katika mfuko wa TANU ili
kufanikisha safari ile. Iddi Faizi ana historia nzuri sana na ni jukumu lao
sasa wanahistoria kuzitafuta habari zake. Iddi Faizi, Sheikh Suleiman Takadir
na Nyerere ndio waliotembea Jimbo la Mashariki mwaka 1958 kuwahamasisha wana
-TANU wasisuse kuingia katika Uchaguzi wa Kura Tatu.
Iwe itakavyokuwa
nyaraka za historia zinaonyesha kuwa alotoa jina la TANU alikuwa marehemu
Abdulwahid Sykes na jina hilo alilitoa Kalieni Camp India mkesha wa Christmas
mwaka 1945 akiwa askari wa 6 Batallion, Burma Infantry katika King’s African
Rifles (KAR) wakati wa Vita Kuu ya Pili. Kalieni Camp ndipo askari wa KAR
walipokuwa wamekusanywa wakisubiri kurudishwa makwao baada ya kumalizika vita. Ukienda
katika shajara yake ya mwaka huo taarifa hizi utazikuta. Juu haya hilo
haliondoi ukweli kuwa huenda na Mzee Bogohe na yeye vilevile alikuwa na wazo la
kuanzisha chama cha siasa hata kama si kile cha
TANU. Ala kuli hali muhimu ni kwa wanahistoria kuwatafuta wazee hawa na
kupokea hazina ambayo si muda mrefu itatoweka.Wangapi leo wanajua kuwa ni Hamza
Mwapachu na Abdulwahid Sykes ndiyo waliomsukuma Nyerere katika ulingo wa siasa?
Au wangapi wanajua historia ya madaktari watano – Dr. Vedasto Kyaruzi, Dr Joseph
Mutahangarwa, Dr Wlibard Mwanjisi, Dr Michael Lugazia na Dr Luciano Tsere na
mchango wao katika kusukuma mbele harakati za TAA kati ya 1948
– 1950?
Kwa kumaliza napenda
kumuuliza msomaji wangu kuwa je, haishangazi kuwa historia ya kutukuka kama hii
ya wazalendo na mashujaa wetu leo imetupwa na haipewi thamani? Kama inashangaza
je, haiwi vyema tukajiuliza kwa nini
imekuwa hivi? Ni nini viongozi wetu wanachokiogopa katika kuwaenzi mashujaa wa
uhuru wa Tanganyika? Je ndiyo tuchukulie kuwa Tanzania ni nchi isiyokuwa na
mashujaa wake? Wasomaji hamkubaliani nami kuwa kuna haja kubwa sana ya kuandika
upya historia ya uhuru wa Tanganyika na kuwaenzi wale wote waliotoa mchango
katika vita vya uhuru? Kwa kumaliza makala haya namshukuru Mzee Lameck Bogohe
kwa kufunua kinywa na kutueleza yale anayoyajua katika kuanzishwa kwa TANU na
kuonyesha kidole kwa yale ambayo ameyaona yanapotosha historia hiyo. Nitafurahi
sana Insha Allah kama watajitokeza wengine na kuandika wanayoyajua kuhusu
mashujaa wetu wa uhuru ambazo habari zao hazijulikani na wengi. Je hapana haja
ya kuiuliza CCM hivi hadi lini wataiacha historia yao inapotoshwa na kupotea?
0 comments:
Post a Comment