Friday 17 May 2013


Nakumbuka zamani niliwahi kusoma kitabu cha hekaya au ngano, vitabu ambavyo wengi tulivisoma bila kutafakari undani wake au maana yake kiujumla.

Kuna simulizi hii ambayo naikumba mpaka leo na nikifananisha na maisha haya ya sasa.
Kijana mmoja alikuwa anaishi na bibi/nyanya yake mzee, kwa bahati mbaya alipokuwa amekwenda kucheza mbali na nyumbani kwao, uku nyuma Dubu aliingia na kumla bibi/nyanya yake, kisha Dubu yule alilala na kujifanya kuwa ndio bibi/nyanya ya yule kijana.

Yule kijana aliporudi mambo yalikuwa hivi:

Bibi mbona masikio yako makubwa?
Bibi akamjibu, ili niweze kukusikia vizuri.
Akamwuliza tena, mbona macho yako ni makubwa?
Akamjibu, ili niweze kukuona vizuri.
Akamwuliza, mbona meno yako makubwa?
Akamjibu, ili niweze kukutafuta vizuri.
Ndipo akaiona miguu yake na dubu yule akamrukia na kumla...

Hiki ni kisa cha kutungwa hakina ukweli wowote ndani yake, ni riwaya ambayo imeandikwa kwa niya ya kuburudisha na kufundisha kidogo. Lakini tukichambua katika uono wa fasihi na kwa undani tunaweza kuifananisha riwaya hii na maisha ya kisiasa.

Dubu huyu anaweza kuwa binadamu yoyote ambaye aidha kwa njia moja ama nyingine tunamwamini, na kumuheshimu. Binadamu huyu ambaye aidha tumempa madaraka au alikuja na kutuomba tumchaguwe ili awe ni mtetezi wetu kwenye Nyanja za siasa na maisha kwa ujumla.

Nasi kwa kumuona kuwa ni mwenzetu na ni mwenye kuonesha kuwa ana masikio makubwa ya kutusikia kilio chetu, na ana macho makubwa ya kuona matatizo yetu, mdomo mkubwa wa kuyasemea matatizo yetu. 
 Lakini tumesahau kuwa Dubu huyu ana meno makubwa ya kutafuna mali asili zetu, kutafuna haki zetu, kutafuna kila anachokiona kuwa anaweza kukitafuna na kusahau kuwa kuna waliomchaguwa ili kusaidia kuwaletea maendeleo.

Matokeo yake kila kilicho kizuri si mali ya taifa tena, bali ni mali binafsi za wanasiasa, wanasiasa ambao tumewapa dhamana ya kulinda maliasili zetu, ili ziweze kutunufaisha sote, matokeo yake kumejengeka matabaka makubwa kati ya wanasiasa na wale wanaoitwa walalahoi.

Hawa ni wananchi ambao vipato vyao havikizi hata matumizi ya wiki moja, pale wanapopata pesa kichele, ambazo zinaitwa mshahara wa kima cha chini. 

Wananchi wanaweza kukubali kupokea kima cha chini na wasilalamike pale tu watakapoweza kumuda maisha yao, watakapoweza kumudu matibabu, kwenye hospitali zenye vifaa vizuri ambavyo mja mzito anaweza kujifungua bila ya kutoa rushwa au kuja na pamba kutoka nyumbani kwake. Mwananchi huyu anaweza asilalamike pale atakapoweza kusomesha watoto zao kwenye shule ambazo walimu wanalipwa vema, ili waweze kufundisha vijana ambao tunawaita ni taifa la kesho...!

Mwananchi anaweza asilalamike pale atakapoweza kula na kunywa vyakula vyenye kuweza kurutubisha afya yake na kumtia nguvu ya kuweza kwenda kuwajibika uko halipo ajiliwa au alipojihajili...!

Lakini haya yote yamekuwa ni ndoto za nchi ya kusadikika, kila kukicha hali inazidi kudorora, utapeli, wizi, ujambazi, umalaya, na halia ya kukata tamaa vinazidi kuongezeka siku hadi siku.

Umefikia wakati sasa kwenye katiba ihainishwe wazi kabisa, kuwa kazi za siasa ndio kazi za wito, malipo yao yawe hayo ya kima cha chini maana wengi wa wanasiasa hatukuwatuma, bali walikuja wenyewe kututaka tuwachaguwe waende kutuwakilisha kwenye ilo linaloitwa Bunge la jamhuri ya muungano.

Kazi za ualimu, udaktari, uhuguzi, Polisi, Majeshi na zinginezo za kuhudumia jamii si kazi za wito ni kazi ambazo wahusika wamezisomea na kuzikeshea usiku ili kupata vyeti. Leo vipi hizo kazi ziwe ni wito, Fikra zangu zinanambia kuwa kazi za Siasa ndio kazi za wito.

0 comments:

Post a Comment

99Graphix

99Graphix
99Graphix
Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!