Tuesday 21 May 2013

Mzee Ally Sykes ni mmoja ya wazee walioshiriki kikamilifu katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika. Alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa chama cha TAA na baadae akawa miongoni wa waasisi 17 walianzisha chama cha Tanganyika African National Union (TANU) tarehe 7.7.1954.

Mzee Ally Sykes ndie aliyebuni jina la Tanganyika African National Union na ndie alitengeneza kadi za mwanzo ambazo ziligawiwa kwa wanachama 17 waanzilishi wa TANU.

Mzee Ally Sykes (wakati huo) akiwa kijana jijini Dar es Salaam ndie alimpokea Mwalimu Julius Nyerere baada ya kukabidhiwa na Hamza Mwapachu na Maharage Juma ambao walikuwa masomoni na Nyerere nchini Uingereza nae akamkaribisha rasmi katika siasa za TAA mwaka 1952 na kushirikiana nae kikamilifu katika harakati za ukombozi wa Tanganyika pamoja na ndugu yake Abdulwahid Sykes ambaye wakati huo ndie alikuwa Rais wa TAA.

Mzee Ally Sykes atakumbukwa kwa juhudi yake, kujitolea kwa hali na mali katika harakati za ukombozi wa Tanganyika. Ingawa hatajwi sana katika historia za waasisi wa taifa hili lakini ukweli unabaki kuwa Mzee huyu pamoja na wazee wengine wengi walikuwa mstari wa mbele na walichangia kiasi kikubwa sana kujenga siasa imara za watanganyika dhidi ya mkoloni Mwingereza na hata taifa hili likajipatia uhuru wake mwaka 1961.

Mzee Ally Sykes amefariki jijini Nairobi nchini Kenya na mwili wake umesafirishwa na kuletwa jijini Dar es Salaam jana Jumapili na maandalizi ya maziko yanafanyika katika Msikiti wa Maamur ulioko Upanga jijini Dar es Salaam ambako maziko yanatarajiwa kufanyika leo Jumatatu 20.05.2013 katika makaburi ya Kisutu.

Ama kwa hakika huu ni msiba kwa taifa hili kumpoteza mmoja ya wazee waliopigania uhuru wa Taifa hili ambao mchango wao uliotukuka kamwe hauwezi kusahaulika kwa vizazi vya wana taifa hili.

"Kama sio juhudi zako Ally Sykes, na uhuru tungepata wapi?"

Taifa limepoteza shujaa, mpigania uhuru na mwasisi wa taifa.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi ameen.



0 comments:

Post a Comment

99Graphix

99Graphix
99Graphix
Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!