Na Mohamed Said

![]() |
Baraza la Wazee wa TANU |

![]() |
Yusuf Halimoja Mwandishi Mkongwe |
Kama
kawaida ya makala za Mzee wangu Yusuf Halimoja huwa ni mchuzi wenye
viungo vingi, hiliki, giligilani, abdalasini, binzari nyembamba na
kadhalika. Mzee Halimoja kazungumza kuhusu historia ya TANU na nafasi ya
Nyerere, kazungumza kuhusu Mihadhara ya “Uchochezi ya Waislam,”
kazungumza kuhusu Elimu ya Waislam na Chuo Kikuu, kama ada yake hakuweza
kuacha kuzungumza kuhusu Waarabu na Utumwa, nk. (Jamhuri 17 23, 2012)
Insha Allah nitajitahidi kugusa kote. Pili ningependa kumfahamisha Mzee
Halimoja kuwa hicho kichwa kilichopamba makala yangu aliyoijibu,
“Halimoja ana Chuki na Waislam,” si kichwa nilichoandika mimi. Nadhani
kichwa hiki ndicho kilichomfanya Mzee Halimoja aseme kuhusu “uchochezi”
wangu. Sasa ikiwa mimi sikuweka kichwa hicho hapo awali ni wazi kuwa
shutuma ya uchochezi itakuwa imeniepuka isipokuwa nitabakia na lile la
kuwaenzi Waislam na mchango wao katika kupigania uhuru wa Tanganyika.
Hata hivyo hilo halinitoi katika kujibu baadhi ya shutuma kuhusu Waislam
kuwa ni “wachokozi.”
Napenda
kumfahamisha Mzee wangu Yusuf Halimoja kuwa kuwa katika maandiko yangu
yote na katika mihadhara niliyopata kutoa ndani na nje ya nchi sijapata
kusema kuwa Waislam walitoa mchango mkubwa kuliko mchango alitoa Nyerere
katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Sijaona haja ya kupima nani
kasaidia zaidi harakati za kudai uhuru labda kwa kuwa hata kama leo
nitataka kufanya hivyo tatizo litakuwa ni vigezo gani nitumie ili kujua
nani kamzidi nani. Hii bila shaka itakuwa kazi kubwa kwa kuwa
walipogania uhuru wa Tanganyika walikuwa wengi. Kuna wale waliokuwa pale
Makao Makuu ya TAA na kasha TANU pale New Street, Dar es Salaam na kuna
wale waliokuwa majimboni. Jingine ni kuwa hadi TANU inaanzishwa TAA
ilikuwa tayari ishakuwapo kwa miaka 21 na viongozi wakiingia na kutoka
na kila mtu alikuwa na mchango wake. Mzee Halimoja akitaka kujua mchango
wa viongozi hawa ambae yeye hawaoni kuwa ni wanasiasa na asome tahariri
alizokuwa akiandika katika miaka ya 1930 ndani ya gazeti lake alilokuwa
kilihariri yeye mwenyewe, “Kwetu.” Nakala za gazeti hili zinapatikana
Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Fiah
alikuwa mfuasi wa Marx na alijaribu kuhamasisha tabaka la wafanyakazi
na wakulima kuwaunganisha dhidi ya ukoloni. Kuanzia mwaka wa 1950
kulikuwa na kamati ya ndani ya TAA iliyokuja kuasisi TANU. Pamoja na
haya kuna viongozi wa Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika waliokujatoa
uongozi katika TANU. Sasa vipi mtu atasema harakati kazianza Nyerere
wakati haya yalipokuwa yakitendeka Nyerere hakuwapo? Kuna wazalendo
kama Kleist Sykes, Ali Jumbe Kiro, Ali Mwinyi Tambwe, Salum Abdallah,
Ibrahim Hamisi, Hassan Machakaomo Maalim Popo Saleh na wengine, hawa
waliitumikia African Association, kasha TAA na baadae TANU. Wengi wao
walishughulika sana katika miaka ya 1940 hadi kumalizika kwa Vita Kuu ya
Pili. Kuna watu kama Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Dossa Aziz
(wanakamati ya ndani ya TAA) waliokuja kupokea kijiti kutoka kwa wazee
wao. Dossa alikuwa hapandi jukwaani lakini ndiyo ilikuwa “benki” ya
TANU. Inasemekana hakuna wa kumfikia Dossa kwa fedha alizotoa katika
kupigania uhuru. Ikutoshe tu kuwa gari la kwanza TANU kuwanalo kumsaidia
Nyerere kwenda huku na kule alilitoa Dossa. Abdulwahid Sykes hakuwa
anapanda jukwaani lakini na yeye alikuwa “sanduku la fedha” la TANU,
halikadhalika mdogo wake Ally Sykes.
Kalamu
ya Abdulwahid Sykes na mipango alokuwa akiipanga akishirikiana Mufti wa
Tanganyika na Zanzibar Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Mwapachu, Dk.
Vedasto Kyaruzi, Stephen Mhando na wanakamati wa TAA Political Sub
Committee ndiyo iliyosababisha uhuru upatikane mwaka 1961. Kamati hii
iliundwa 1950 ndani ya TAA na wakati ule Nyerere hakuwapo. Vijana hawa
walikungwa mkono na wazee waliounda Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa
na Waislam watupu. Katika hawa wazee wapo waliokuwa wanapanda majukwaani
na kusafiri na Nyerere vijijini kuitangaza TANU kama Sheikh Suleiman
Takadir, Rajab Diwani na wengineo na walikuwapo wengine hawakuwa wapanda
majukwaa lakini wakichangia juhudi zile kwa njia nyingine. Katika hawa
mchango wa Mshume Kiyate ni wa kupigiwa mfano. Harakati za kudai uhuru
hazikuanza na Nyerere mwaka 1954 vuguvugu lilianza toka miaka ya mwisho
ya 1920 African Association ilipoasisiwa. Chama hiki kina historia yake
na kina mashujaa wake waliofanya makubwa, katika wakati wao kama Kleist
Sykes, Erika Fiah, Ali Juma Ponda, Hassan Tawafiq Suleiman, Edward
Mwangosi na wengine wengi. Wazalendo hawa walikuwa na mchango wao wa
kuwaamsha wananchi wajijue.
Naamini
Mzee wangu Halimoja labda hakuwa anayajua haya kama Watanzania wengi
walivyokuwa gizani katika historia hii ya kutukuka. Mzee Halimoja yeye
anaamini hapakuwa na siasa katika TAA lakini Waingereza wakijua fika
kuwa TAA ingawa haikuwa na katiba ya siasa lakini kilikuwa chama cha
siasa kamili. Moja ya masikitiko yangu ni kuwa hadi leo watoto wa
marehemu Abdulwahid Sykes hawajaamua kuzifungua na kuziweka wazi shajara
zake alizokuwa akiziandika wakati kabla na baada ya kuunda TANU kwa
hiyo mengi hayajulikani kama ambavyo tungelipendfa kufahamu. Ningependa
kumwekea msomaji hapa machache kutoka nyaraka za Sykes:
"...it is reported that the Secretary of the Association, Abdul Wahid Sykes has
dispatched letters to all branches asking members for suggestions under
the following heads for a memorandum to be prepared for the Royal
Commission..."
“...Abdul Wahid Kleist Sykes, Secretary of the African Association who, as
reported in last month's summary (paragraph 20) was going on safari up
country, visited Mwanza, where he met Paul Bomani, President of the
Bukoba African Association, and accompanied him to Bukoba. Sykes then
visited Kampala alone.....on 8th March, a secret meeting was held, attended
by leading members of the Mwanza Branch...”
by leading members of the Mwanza Branch...”
(Tanganyika Political Intelligence Summary March, 1952).
Tukija katika TAA hasa kuanzia mwaka wa 1950 kuna wengi waliopambana na ukitaka kujua hali ya siasa ilivyokuwa wakati ule pitia nyaraka za marehemu Abdulwahid Sykes. Utakayosoma katika nyaraka hizi zitakudhihirishia bila hofu wala wasiwasi kuwa TAA kilikuwa chama cha siasa. Kutokana na nyaraka hizi mwandishi ameandika kitabu cha maisha ya Abdulwahid Sykes na ndani yake kawataja wale wote walioondolewa aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya katika historia ya kudai uhuru. Inawezekana watu kama Halimoja hawataki tu kusikia upande mwingine wa historia. Hili ni jambo la kusikitisha kwani kwa kuifunga akili yao kuhusu historia hii watapitwa na mengi. Halimoja anasema Nyerere ndiye aliyepeleka harakati vijijini. Halimoja anasema hivyo kwa kuwa labda kama ni mkweli kuna asiyoyajua kuhusu kuipeleka TANU kwa wananchi. Ushahidi wa kihistoria haukubaliani na msimamo wa Mzee Halimoja. Ningependa kumkumbusha Mzee Halimoja majina ya waasisi wa African Asociation kwa kuwa yeye kanasa na Cecil Motola peke yake mtu wa Masasi mwenzake. Kleist Sykes ndiye aliyeasisi Africa Association baada ya kuifanyia kazi fikra aliyopewa na Dr. Aggrey mwaka 1924. Kleist aliasisi African Association mwaka 1929 akiwa na rafiki zake wa karibu kama Mzee bin Sudi, ambaye wazazi wake walikuwa Wamanyema kutoka Belgian Congo, Ibrahim Hamis - Mnubi ambaye baba yake alitoka Daffur nchini Sudan, Zibe Kidasi, Ali Said Mpima - Mzaramo, Suleiman Majisu, Raikes Kusi, Rawson Watts na Cecil Matola - Myao kutoka Masasi, Kleist akiwa katibu muasisi wa African Association.
Napenda
tena kumjuvya Mzee Halimoja kuwa wanachama wa kwanza wa TANU walitoka
Rufiji mwaka 1954 na aliyekwenda kuwatafuta wanachama hao ni Said
Chamwenyewe baada ya kuagizwa na Abdulwahid Sykes ili TANU ipate tasjila
kwa kuwa wakoloni walikataa kuisajili TANU ati chama hakina watu.
Katika kipindi hicho majuma machache tu tangu TANU iasisiwe Zuberi
Mtemvu akachukua kadi za TANU kutoka kwa Ally Sykes akifuatana na
Nyerere wakenda Morogoro kukitangaza chama. Mwaka 1956 katika vijiji vya
Dodoma TANU iliingizwa vijijini na Haruna Taratibu na Omar Suleiman.
Mwaka huo huo katika vijiji vya Jimbo la Kusini, TANU iliingizwa
vijijini na Salum Mpunga, Yusuf Chembera, Suleiman Masudi Mnonji,
Shariffa bint Mzee, Said Alley Mwalimu, Mohamed Ali Abdallah na
wanaharakati wengine. Huko Kilimanjaro TANU ilienezwa na akina Yusuf
Olotu, Mama bint Maalim, Halima Selengia, Melkezedek Saimon, Gabrieli
Malaika, Eikaeli Mbowe, Juma Ngoma na wengine wengi. Mifano naweza
kuitoa mingi sana.
Halimoja
anasema labda kwa kegemea historia ya Nyerere kama aijuavyo yeye kuwa
tawi la Dar es Salaam la TANU ndilo lilikuwa dhaifu. Sijui anakusudia
tawi lipi kwa kuwa matawi ya TANU Dar es Salaam yalikuwa lukuki na yote
hayo yalikuwa na nguvu sana kuanzia Makao Makuu New Street hadi uje Tawi
la Kisutu ambalo baadae lilikuja kuhamia Mtaa wa Mvita. Hili tawi la
Mvita lilikuwa chini ya uongozi wa Mtoro Kibwana kama katibu na Sheikh
Haidar Mwinyimvua kama Mwenyekiti na baadae uenyekiti ukashikwa na Yahya
Saleh. Inasemekana tawi hili ndilo lililokuwa na nguvu kushinda matawi
yote Tanganyika. Huu ndiyo ukweli na picha na nyaraka kuthibitisha haya
yote zipo na mwandishi katika kutafiti historia ya uhuru wa Tanganyika
kapata bahati ya kuzisoma nyaraka za wakati huo na kuzifanyia uchambuzi.
Sasa kama Mzee Halimoja bado kaelemewa na ile propaganda kuwa TAA
kilikuwa chama cha starehe hakuna wa kumzuia katika fikra zake hizo. Kwa
mukhtasari hii ndiyo ilikuwa michango ya baadhi ya wazalendo ambao hadi
leo taifa limewasahau. Katika hali kama hii vipi Mzee Halimoja atadai
kuwa Nyerere alikuwa na mchango wa pekee? Hiyo pekee kama ipo na
ataufahamishe tupo tayari kumwazima masikio yetu.
Nampa
chamgamoto Mzee Halimoja aeleze ni akina nani waliingiza TANU Peramiho
na Masasi. Mtu mmoja asingeweza kupigana vita ile peke yake. Nyerere
hakuwa peke yake si Dar es Salaam wala huko vijijini alikosema Mzee
Halimoja. Tabu ya wanaotaka kumtukuza Nyerere peke yake kama Mzee
Halimoja iko hapa. Wao hawawataki kabisa kusikia historia ya
waliomtangulia Nyerere katika siasa au aliokuwanao pamoja bega kwa bega.
Hamu yao kubwa ni kuwa historia ya uhuru wa Tanganyika ianze na
kumalizikia kwa Nyerere. Iwe itakavyokuwa mimi sina ugomvi na wao kila
mtu ana uhuru wa mawazo yake hatulazimishani katika hilo. Jambo la
kushangaza ni kuwa anapokuja mtu na maelezo mengine ya historia ya kudai
uhuru hawa wenzetu wanaumwa sana. Ninachosema siku zote ni kuwa uhuru
wa Tanganyika umepiganiwa kwa kiasi kikubwa sana na Waislam na jambo la
kusikitisha hao walioupigania uhuru huo bega kwa bega na Nyerere
hawatambuliwi na hawajapewa heshima na hadhi wanayostahili. Haya ndiyo
mambo mawili ambayo nimekuwa nikikisisitiza siku zote.
Sasa
tuje suala la mihadhara. Historia ya mihadhara ni ndefu na inahitaji
makala maalum ili kuitendea haki. Wachungaji walikuwa wakipita katika
nyumba za Waislam kuwahubiria wakumkubali Yesu ili waokoke. Hili
limekuwa likifanyika kwa zaidi ya miaka mia sasa. Kuna kisa maarufu cha
Sheikh Idrissa bin Saad na padre kutoka kanisa la Misheni Kota
aliyekuwa akija nyumbani kwa Sheikh Idrissa kumuhubiria “Neno la Bwana.”
Inasemekana Sheikh Idrissa alikuwa akimkaribisha huyu mchungaji na
akiagiza chai iletwe kwa jili ya mgeni wake na sheikh akikaa kimya
kumsikiliza hadi amalize mahubiri yake kisha wanaagana. Wanafunzi wa
sheikh walikuwa wakikereka sana na hali ile lakini Sheikh Idrissa
alikuwa akiwaeleza kuwa dini inahitaji ustahamilivu. Kwa muda mrefu sana
mahubiri ya dini yalikuwa yakifanywa na Wakristo peke yao na kwa kweli
mihadhara hiyo haikuwa na athari yoyote kwenye Uislam. Matatizo yalianza
pale Waislam kuanzia miaka ya mwanzo 1990 nao walipoanza kutoka
misikitini na kuutangaza Uislam hadharani wakitumia Biblia. Baada ya
mihadhara hii huko Sumbawanga Wakristo 2000 kutoka Kanisa Katoliki
walisilimishwa na Kagera Padri Yusufu Makaka wa Kanisa la Kilutheri
Kagera yeye na wafuasi wake 3000 walisilimu na kuingia Uislam. Hofu kuu
iliingia katika kanisa na hawakuwa na pa kwenda isipokuwa kuomba msaada
wa seriakali ilihami kanisa lisije likasambaratika. Kadinali Otunga wa
Kanisa Katoliki Kenya yeye alitoa ilani kwa kusema kuwa kanisa lipo
katika hali ya kusambaratishwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa
kulihami dhidi ya wahubiri wa Kiislam. Kufuatia matokeo haya mwaka 1989
Christian Council of Tanzania (CCT) iliionya serikali kuhusu wahubiri wa
Kiislam. Mwaka 1993 Tanzania
Episcopal Conference (TEC) ikatoa taarifa yenye vitisho kuwa endapo
Waislam hawataacha mahubiri yao damu itamwagika. Mapdri walijaribu
kupambana na wahubiri wa Kiislam juu ya ulingo lakini walikuwa
wanashindwa vibaya sana. Hilo ndilo lilowafanya wakimbilie kutoa vitisho
na kutaka msaada wa serikali kuwadhibiti Waislam. Mtokeo ya juhudi hizi
za kanisa ni mauaji ya Mwembechai mwaka 1998. Hii ndiyo hali ya mambo
kwa mukhtasari.
Mzee
Halimoja kaeleza habari ya Waarabu na utumwa. Hakuna wa kupinga hilo
kuwa Waarabu walishiriki katika biashara ya utumwa kama vile
walivyoshiriki Wazungu na Waafrika. Hata hivyo ningependa kumzindua kuwa
mbona kawataja Waarabu peke yao katika biashara hii? Kwani yeye hajui
kuwa kulikuwa na biashara ya utumwa kupitia bahari ya Atlantic na meli
moja ya kubeba watumwa ilikuwa ikiitwa “Jesus?” Mzee Halimoja kaeleza
Waislam kukosa chuo kikuu hadi walipopewa na Benjamin Mkapa. Kisa cha
East African Muslim Welfare Society (EAMWS) na kupigwa kwake marufuku na
Nyerere ni katika mambo maarufu kwa Waislam. Mzee Halimoja anatonesha
kidonda. Nyerere aliihujumu jumuia hiyo ya Waislam kwa kuwa ilikuwa
ikijenga Chuo Kikuu. Mkapa akitumia gazeti la Nationalist, Martin Kiama
akitumia Radio Tanzania, Geofrey Sawaya wa Jeshi la Polisi walikuwa
washiriki wakuu wa katika kampeni ile dhidi ya EAMWS mwaka 1968 kama
lilivyokuwa Kanisa Katoliki wakimtumia Nyerere. Hii ni mada ya
kujitegemea Insha Allah itakapopatikana nafasi tutazungumza kwa marefu
na mapana yake.
Juu ya hayo yote Tanzania ni nchi huru watu wana uhuru wa kumpachika yeyote wampendae jina wanaloona linamwenea ama liwe “Baba wa Taifa,” “Baba wa Kanisa” nk. Mtu huwezi kuwa na ugomvi na mambo kama haya. Leo kuna maprofesa wala hawajauona mlango wa darasa na maprofesa hawajaenda mahakamani kuweka p;ingamizi wala wenye shahada zao hawajaonesha kukereka. Ukipenda unaweza hatakuwa Field Marshal na hakuna atakaekuuliza wapi ulipigana vita na katika jeshi lipi. Halikadhalika mtu ana uhuru wa kuamini historia yoyote aitakayo. Anaweza kudai kuwa TANU ilianzishwa na Nyerere mwaka 1954 na akaja mwingine akasema hilo haliwezekani na kama kuna mzalendo anaeweza kujinasibu na kuanzishwa kwa TANU basi marehemu Abdulwahid Sykes anastahili zaidi kwani baba yake ndiye aliyeasisi African Association mwaka 1929 na kati ya 1930 hadi 1933 akajenga ofisi ya African Association New Street, nyumba ambayo TANU ilikuja kuzaliwa ndani yake mwaka 1954.
Siwezi kumjibu Mzee Halimoja kila alosema hapa tulipofika panatosha.
19 Januari, 2012
19 Januari, 2012
Sheikh Nurdin Hussein Khallifa wa Tariqa Shadhliy |
![]() |
Ali Juma Ponda |
Erika Fiah |
0 comments:
Post a Comment