Tuesday 4 February 2014

Na Mohamed Said 
Kwa hakika ni kitendawili kikubwa ikiwa utakaa chini na kuwaza kuhusu historia ya TANU. Wanahistoria wetu wamewapuuza kabisa wazalendo waliokuwakatika harakati kabla ya Nyerere. 

Binafsi nimeulizwa maswali mengi katika kila muhadhara niliofanya ndani na nje ya nchi kuhusu mchango wa Nyerere katika kuunda TANU. Wanataka kujua palipitika nini hata ikawa TANU inanasibishwa na Nyerere peke yake? Wakati mwingine hutoa jibu na wakati mwingine nikiwa nimechoka husema swali hilo lielekezwe kwenye CCM (Chama Cha Mapinduzi) kwa kuwa wao ndiyo warithI wa TANU. Kama wamerithi TANU basi watakuwa wamerithi na historia yake. Miaka michache iliyopita palikuwa na mjadala mkali sana katika Jamii Forum kuhusu hili. Nimepita katika kumbukumbu zangu na nimekuta jibu nililotoa kwa mmoja wa wanajamvi wa JF. Ningependa na wasomaji wangu nanyi muone nilisema nini.

Hali ya TAA Makao Makuu New Street, 1950

Kueleweka kwa nini Abdulwahid alimuunga mkono Nyerere inahitajika uchambuzi kuelewa siasa za mfumo wa kikoloni katika Tanganyika. Mwaka wa 1951 Abdulwahid Sykes na Hamza Mwapachu walipokuwa wakishughulika kuifufua TAA, walijiwa na Ivor Bayldon, [1] Brig. Scupham na V.M. Nazerali kuombwa kuunga mkono kuundwa kwa chama cha kisiasa kitakachojumuisha Watanganyika wa rangi zote. Hawa walikuwa wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria. Bayldon alikuwa mlowezi tajiri kutoka Nyanda za Juu za Kusini na alikuwa amehamia Tanganyika kutoka Afrika ya Kusini. Wajumbe wa Kiafrika wa Baraza la Kutunga Sheria walioliunga mkono wazo hili walikuwa Chifu Kidaha Makwaia na Liwali Yustino Mponda wa Newala [1]. Watu wengine mashuhuri walioshauriwa na kuombwa kuunga mkono chama hiki walikuwa: Dr Joseph Mutahangarwa, Chifu Abdeli Shangali wa Machame, Chifu Mkuu Thomas Marealle wa Marangu, Chifu Adam Sapi Mkwawa, Chifu Haruna Msabila Lugusha, Dr Wilbard Mwanjisi, Abdulkarim Karimjee, Dr Vedasto Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K. Viran, Stephen Mhando, Ally Sykes na Dossa Aziz [1].

Huu ulikuwa mchanganyiko wa Wazungu ambao tangu hapo walikuwa raia wa daraja la juu, baadhi yao kama Bayldon walikuwa walowezi; machifu  kama vile Marealle, Waafrika wasomi  kama Mwapachu; tabaka ya wafanyabiashara wa Kiasia kama Karimjee na watu wa mjini kama Dossa Aziz na Juma Mwindadi.  Wote hawa walikuwa viongozi waliokuwa na wafuasi katika jumuiya zao. Katika barua Nazerali aliyomtumia Ally Sykes miaka miwili baada ya kudhihiri kuwa chama kile walichokusudia kisingeweza kuundwa, Kwenye sehemu moja alikuwa na haya ya kueleza: ëHaja kubwa ilikuwa kuandaa kikundi cha watu walio wakweli, waaminifu na wenye imani katika maendeleo ya watu katika nchi yetu, pamoja na fursa sawa kwa wote.

Abdulwahid wakati huo akiwa katibu pamoja na wanachama wa TAA wasingeweza kukubali wazo kama hilo. Ingawa kwa kiasi fulani malengo ya chama hicho kilichokusudiwa yalionekana yanafanana na malengo ya wananchi hivyo kudhihirisha barabara kile ambacho TAA ilikuwa ikikipigania, Waafrika wasingeweza kuachia azma ya wa Tanganyika kwa dhamira njema ya wasiokuwa Waafrika na ambao walikuwa wakishirikiana bega kwa bega na serikali ya kikoloni. Ilikuwa dhahiri kuwa Wazungu na Waasia nchini Tanganyika hawakutaka kukubali kuwa Tanganyika kwa hali yoyote ile ilikuwa nchi ya Waafrika. Kwa TAA kukubali kuundwa chama cha siasa kitakachojumuisha mataifa yote, kulikuwa sawa na kuyaweka maslahi ya Waafrika chini ya watu wachache. Miaka michache nyuma wazo kama hilo chini ya kile kilichojulikana kama Capricon Society lilianzishwa na wakoloni katika maeneo ya Tabora ambako kulikuwa na idadi kubwa ya Waafrika wasomi, wengi wao wakiwa Waalimu. Imani ya Capricon Society ilifungamana na dhana ya ëuhuru kwa Waafrika waliostaarabikaí. Stephen Mhando aliyekuwa Dar es Salaam na akiwasiliana na George Magembe mjini Tabora alituma barua kwa uongozi wa TAA huko akiwatahadharisha juu ya mtego wa na Capricon. Ilikuwa dhahiri kuwa Tanganyika wakati ule ilikuwa ikitafuta mwelekeo wa kisiasa na haikuwa TAA peke yake iliyokuwa ikishughulika kutaka kuonyesha njia.

Mara baada ya Nyerere kuchukua uongozi wa TAA chama kikaanza kusinzia, ushupavu na bidii iliyokuwepo wakati wa  uongozi wa Abdulwahid vilitoweka. Kwa hakika ilikuwa wakati mmoja tukatika historia ya Dar es Salaam ambapo mkristo Erikah fia, alikamata bendera dhidi ya serikaly ya kikoloni. Nyerere alikuwa akikaa nje ya mji na alikuwa akija Dar es Salaam mwishoni mwa juma tu. Kwa kiasi fulani hii iliathiri shughuli za chama. Kwa muda wanachama walionekana kama wamepoteza hamu ya chama. Wajumbe wa kamati ya utendaji mara nyingine hawakutokea kwenye mikutano ijapokuwa Dossa aliwapitia majumbani kwao na gari yake kuwachukua.

Dossa anakumbuka kuwa alikuwa akisimama nje ya nyumba ya mwanakamati na kupiga honi. Mtoto au mke wa mwanakamati angetoka mlangoni kutoa habari kuwa hakuwapo, katoka ilhali yupo ndani. Kwa muda kidogo ilionekana kama Nyerere alikuwa kikwazo cha maendeleo ya TAA. Na huu ndiyo ulikuwa mwendo wa TAA, nguvu yake ilikuwa ikitegemea uwezo wa viongozi wake. Awamu ya kwanza ya uongozi wa Kleist Sykes na Mzee Bin Sudi katika makao makuu TAA ilipiga hatua kubwa. Vivyo hivyo katika zama za Ali Juma Ponda na Hassan Suleiman katika tawi la Dodoma, TAA ilikuwa ikisikika sana na uongozi wake uliheshimiwa hata nje ya Tanganyika. Abdulwahid alikuwepo kama makamu wa rais lakini alipendelea kumwona Nyerere akiendesha ofisi na kufanya maamuzi yake mwenyewe kama rais. Akakihofia kufa kwa chama, Abdulwahid aliwataka shauri viongozi wenzake wa ndani katika TAA - Ally, Dossa, Tewa na Rupia kuwa kipi kifanyike ili kudhibiti hali ile iliyojitokeza. Ilikuwa dhahiri tatizo lilikuwa ni katika kubadilisha uongozi. Wanachama walikuwa hawana imani na uongozi mpya katika ngazi ya juu. Hili linaweza kueleweka ikifikirika kuwa ilikuwa ni miaka mitatu tu huko nyuma wakati Abdulwahid na Dr Kyaruzi walikifufua baada ya kupoteza mwelekeo baada ya Vita Kuu ya Pili. Iliamuliwa kuwa wazee Waislam wa mjini Dar es Salaam waombwe kumuunga mkono Nyerere.

Wazee walifatwa na wakaelezwa kuwa uongozi wa TAA ulikuwa umemkubali Nyerere kama rais wa chama kama sehemu ya mpango wa kuigeuza TAA kuwa chama cha siasa cha umma  Abdulwahid aliwaeleza wazee, miongoni mwao masheikh, kuwa nchi ilikuwa katika awamu yake ya mwisho ya harakati ambayo ilihitaji kuungwa mkono na kila Mwafrika wa Tanganyika bila kujali dini yake wala kabila. Hawa wazee walikuwa wanachama wa TAA lakini vilevile walikuwa wanachama au viongozi katika vyama vyao vya kikabila kama vile Batefera Union chama cha Wamanyema kilichokuwa kikiongozwa na Mzee bin Sudi, na Zaramo Union chini ya uongozi wa Makisi Mbwana. Baadhi ya wanachama waliokuwa katika vyama hivi walikuwa vilevile wanachama wa Al Jamiatul Islamiyya. Abdulwahid aliwaambia wazee kuwa makao makuu ya TAA yaliwahitajisana kuunga mkono chama, pamoja na wasomi kama Julius Nyerere waliochukuliwa kuwa watiifu kwa utawala wa kikoloni.  Hawa wanaodhaniwa kuwa watiifu kwa utawala wa kikoloni ndiyo wanaofaa sana kugeuzwa waipinge serikali inayowadhulumu wananchi.

Wazee waliafiki ushauri huu na wakaanza kumjenga Nyerere kama kiongozi wa kuwasemea na kuwaunganisha Waafrika wote wa Tanganyika. Mwanafunzi mmoja wa Mufti Sheikh Hassan bin Amir anakumbuka kuwaona Abdulwahid, Dossa Aziz na Nyerere mara kadhaa katika miaka ya mwanzoni ya 1950 wakija kuonana na sheikh katika madrassa yake Kariakoo, Amani Street, nyumba nambari 36. Kwa kawaida Abdulwahid, Dossa Aziz na Nyerere walipokuja kumwona Mufti, Sheikh Hassan Bin Amir alikuwa akivunja darsa na kuwapa ruhusa wanafunzi wake ili upatikane utulivu wa maongezi. Kwa kawaida mashauriano yalikuwa yakifanyika mle mle ndani ya madrasa, Abdulwahid, Dossa na Nyerere wakiwa wamekaa chini kwenye jamvi wamekunja miguu. Wazee wengine mashuhuri waliomuunga mkono Nyerere walikuwa Sheikh Suleiman Takadir mwanachuoni wa Kiislamu aliyeelimika sana, akijulikana zaidi kwa jina la utani ëMakariosí, Jumbe Tambaza, mzee aliyekuwa akihodhi ardhi kubwa pale mjini; Mshume Kiyate, mzee muuza samaki aliyekuwa na kipato kizuri; Mwinyijuma Mwinyikambi, mzee aliyekuwa na viunga vya minazi na miembe; Rajabu Diwani, seremala hohe hahe lakini aliyejaaliwa ufasaha mkubwa wa kuzungumza; Makisi Mbwana, kiongozi wa Wazaramo mjini Dar es Salaam; Sheikh Haidari Mwinyimvua, fundi cherehani na mtu mwadilifu; Iddi Faizi Mafongo na Idd Tosiri ndugu wawili Wamanyema na binamu wa Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo Khalifa wa tariqa ya Qadiriya. Iddi Faizi akiwa mweka hazina wa Al Jamiatul Islamiyya na Iddi Tosiri mwanachama shupavu); Iddi Tulio, mzee mwenye heshima zake, Mashado Ramadhani Plantan, mhariri na  mmiliki wa gazeti la Zuhra na kaka yake Schneider Abdillah Plantan, watoto wa Affande Plantan na wazee wengine wengi wa mjini.

0 comments:

Post a Comment

99Graphix

99Graphix
99Graphix
Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!