Friday 27 December 2013

WALIOACHA ALAMA KATIKA HISTORIA YA TANU

Na Mohamed Said
 Katika kitabu changu ''The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924 - 1928) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism'' London 1998,  ambacho kilikuja kufasiriwa na kuitwa ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes Historia iliyofichwa  Kuhusu Harakati za Waislam Dhidi ya Ukoloni wa Waingereza'' Nairobi 2002 nimeandika maneno hayo hapo chini kuhusu Dome Budohi:

''Familia yangu ilifahamiana na Dome Budohi, mmoja wa wanaharakati kutoka Kenya. Wakati ule wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika alikuwa akiishi Dar es Salaam. Budohi alikuwa mmoja wa wazalendo walioasisi TANU na kadi yake ya uanachama ni nambari sita aliyopewa Julai 1954. Mwaka 1955 alikamatwa na serikali ya kikoloni kwa tuhuma ya kuwa mmoja wa askari wa Mau Mau harakati za wazalendo takriban wengi wao wakulima wadogo waliokuwa wakipigana na ukoloni wa Waingereza nchini Kenya. Ninazo kumbukumbu nyingi za utoto nikimtembelea Budohi ndani ya selo yake Kituo Cha Kati cha Polisi. Hivi sasa jengo hilo ni Makao Makuu ya Shirika la Reli la Tanzania. Wakati huo mimi nilikuwa mtoto, si zaidi ya miaka minne hivi. Jambo la kwanza ninalokumbuka kuhusu Budohi ni kuwa kila mara tulipokwenda kumtembelea tulimkuta anasoma gazeti. Baadae Budohi alihamishiwa Kenya na aliwekwa kizuizini katika kisiwa cha Lamu. Alipofunguliwa toka kizuizini mwaka wa 1963 miezi michache kabla ya uhuru wa Kenya, Budohi alikwenda Uganda na akaajiriwa na gazeti la Uganda Argus. Hivi sasa ninaelewa kwa nini siku zile kila mara nilikuwa namkuta amezama ndani ya gazeti kila tulipokwenda kumtembelea pale rumande mjini Dar es Salaam. Niliweza kwa msaada wa rafiki yake Maxwell aliyelowea Tanganyika, kumpata Budohi mjini Nairobi mwaka 1972. Nilimtembelea mjini Nairobi wakati huo alikuwa akiishi Ruiru maili chache kutoka Nairobi mjini. Budohi alikuwa ametundika picha ya Nat King Cole sebuleni kwake. Mwaka 1974 nilimtembelea tena, safari hii katika nyumba yake ya Ngei Estate. Budohi alikuja kuwa mtu wa kwanza kabisa kunipa habari kuhusu historia ya harakati za Tanganyika dhidi ya ukoloni wa Waingereza. Hata hivyo wakati ule nilikuwa bado sijapata hamu wala kuwa na hamu ya kuandika kitabu kuhusu uhuru wa Tanganyika.

Kulikuwepo na wazalendo kutoka nchi jirani ya Kenya kama vile Dome Okochi Budohi na Patrick Aoko ambao walikuwa wanajua vyema siasa za walowezi za kupora ardhi za  wananchi. Kutoka kwa wazalendo kama hawa, Abdulwahid alipata usikivu wa mawazo yake ya kuigeuza TAA kuwa chama cha siasa chenye nguvu. Lakini mara tu baada ya kuundwa kwa TANU wazalendo hawa wa Kenya wakakamatwa na serikali. Kwa miezi sita walihojiwa na kuwekwa rumande Central Police Station huku wamefungwa minyororo. Budohi na Aoko walikuwa wakifuatwa na makachero (Special Branch) toka mwaka wa1952 baada ya hali ya hatari kutangazwa Kenya. Inasemekana Dome Budohi aliponzwa na barua iliyotoka Kenya ambayo ilikamatwa na makachero. Barua hii ilikuwa inamuhusisha Budohi na Mau Mau. Inasemekana Budohi alisalitiwa na Mkenya mwenzake aliyeitwa Martin[1] ambaye alikuwa pamoja naye katika Blackbirds. Martin alikuwa akipuliza tarumbeta.

Askari waliokuwa wakiwalinda kule rumande walitoa habari kwa TANU kuwa kulikuwa na mpango wa kuwapa sumu wafungwa wale, Budohi na mwenzake Aoko. Baadaye wafungwa hawa walihamishiwa Handeni ambako kulikuwa na kambi ya kuwafunga watuhumiwa wa Mau Mau. Kawawa alikuwa amehamishiwa hapo kutoka Dar es Salaam. Baadhi ya wafungwa walikuwa wananachama wa TAA na baada ya kuundwa TANU wakawa wanachama wa TANU. Kawawa alikuwa akifahamiana na wengi kati ya wafungwa wale. Budohi na Aoko waliwahi kuwa  viongozi wa TAA. Kawawa aliwaangalia wafungwa hawa kwa moyo wa huruma akijaribu kupunguza shida zao pale kambini kila alipopata mwanya wa kufanya hivyo. Budohi aliwahi kucheza senema ya Kiswahili na Kawawa iliyoitwa Mgeni Mwema iliyokuwa imetayarishwa na Community Development Department. Idara hii ilitengeneza filamu kadhaa ambazo Kawawa alicheza kama nyota wa mchezo. Katika senema zote alizocheza, iliyopata umaarufu na kupendwa zaidi ilikuwa Muhogo Mchungu ambalo ndiyo lilikuwa jina la Kawawa katika filamu hiyo.

Minongíono ilikuwa ikisikika kutoka kanda ya ziwa kuwa kiongozi wa wapiganaji wa Mau Mau, Dedan Kimathi alikuwa anaonekana mjini Mwanza. Wakati ule pale Mwanza kulikuwa na Wakikuyu wengi wakifanya biashara sokoni. Ilivumishwa kuwa Dedan Kimathi alikuwa akiwasiliana na Wakikuyu wenzake na wao walikuwa wakimkusanyia fremu za baiskeli za zamani ili zitumike kutengenezea magobole ili zitumiwe misituni dhidi ya majeshi ya Waingereza. [1]  Mapigano yalipoonza kati ya Mau Mau na Waingereza kulikuwa na Wakikuyu kama elfu kumi na sita wakiishi na kufanya kazi kaskazini ya Tanganyika. Kama tahadhari, Wakikuyu wachache walioonekana kuunga mkono Mau Mau, walikamatwa na kupelekwa Kenya ambako waliwekwa kizuizini katika kambi mbali mbali. Wakati Budohi na Wakenya wengine walipopita Korogwe wakati wakirudishwa Kenya kupitia Taveta, Ally Sykes, ambaye alikuwa amehamishiwa Korogwe, alikwenda hadi stesheni ya reli kuwaaga. Watuhumiwa hawa wa Mau Mau walikuwa wametiwa katika mabehewa ya kubebea ng'ombe huku wamefungwa minyororo. Dome Budohi na wazalendo wengine waliwekwa kizuizini kwa miaka saba.

Katika wale walioasisi TANU, ni wale tu aliokuwa makao makuu ya TAA ndiyo wanaoweza kueleza historia ya kweli ya  chama hiki. Hawa ni John Rupia, Dossa Aziz, Tewa Said Tewa, Julius Nyerere, Dome Budohi, Abdulwahid na Ally Sykes.

Miaka mingi baada ya kutoka kizuizini kisiwa cha Lamu, Budohi bado alikuwa ma mfundo na Martin na kila alipozungumza kuhusu yeye na mwandishi,alionyesha chuki ya kupindukia.

Wazalendo wa Kenya waliokuwa katika harakati nchini Tanganyika hawakuwa na uhusiano na TANU baada ya uhuru na wala chama hakikufanya juhudi kuwasiliana nao. Dome Budohi alijaribu mara nyingi kuomba kukutana na Nyerere alipozuru Nairobi lakini ilishindikana. Budohi hafahamu kama maafisa wa serikali ya Tanzania walimzuia wao tu au walifanya hivyo kwa amri ya Nyerere. Hadi anafariki Dome Budohi hakuwahi kuonana na Nyerere ambae wakati wa enzi za TAA na TANU walikuwa wakifahamiana vizuri.

Kadi nambari 1 ilitolewa na Ally Sykes kwa rais wa TANU, Julius Kambarage Nyerere na Ally aliweka sahihi yake kama afisa aliyeitoa. Ilipendekezwa kwamba kadi chache za mwanzo lazima zipigwe mnada na fedha zitakazokusanywa zitiwe  kwenye hazina ya chama. Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na wengine walipanda dau kununua kadi hizo. Ally alimshinda kaka yake Abdulwahid kwa bei akapata kadi ya TANU nambari 2; Abdulwahid alipewa kadi nambari 3; Dossa Aziz kadi nambari 4; Phombeah kadi nambari 5; Dome Okochi, mmoja wa wale wazalendo kutoka Kenya katika TANU alipata kadi nambari 6 na Rupia kadi nambari 7. Bibi Titi kadi nambari 16; Iddi Tosiri kadi nambari 25.

Mwezi June 1953, makao makuu ya TAA yalitangaza kamati yake ya utendaji: J. K. Nyerere, Rais, Abdulwahid Sykes, Makamu wa Rais; J. P. Kasella Bantu, Katibu Mkuu; Alexander M. Tobias na Waziri Dossa Aziz, Katibu wa pamoja wa muhtasari; Wajumbe wa kamati: Dr Michael Lugazia, Hamisi Diwani, Tewa Said Tewa, Denis Phombeah, Z. James, Dome Okochi, C. Ongalo na Patrick Aoko.[1] Muundo wa uongozi katika TAA unaonyesha ule mshikamano wa Afrika ya Mashariki uliokuweko wakati wa harakati za uhuru. Wazalendo wa Kenya walichaguliwa kama viongozi wa TAA bega kwa bega na Watanganyika.''

Nimenyanyambua vipande hivyo kutoka sehemu tofauti ya kitabu changu ili kutoa picha na kujaza habari katika historia ya TANU na harakati za kudai uhuru. Mengi ya haya hayajulikani na wengi na hivyo kuathiri sana kufahamika na kuheshimu historia ya uhuru wa Tanganyika na mashujaa wake.


 

0 comments:

Post a Comment

99Graphix

99Graphix
99Graphix
Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!