Thursday 26 December 2013

SIASA KATIKA MJI WA DAR ES SALAAM MIAKA YA 1950


Naikumbuka Gerezani kama vile ilikuwa jana. Kuanzia mitaaa yake hadi nyumba zilizokuwapo pale pamoja na wakazi wake ambao kwangu mimi walikuwa baba, mama, shangazi zangu na wajomba ukiachilia watoto wa rika langu tuliokua tukicheza pamoja. Mitaa takriban yote ilikuwa ni barabara za vumbi tupu lakini mchanga. Kwa sisi watoto hii ilikuwa afueni maana tuliweza kucheza tukakimbizana bila ya madhara ya kuumia sana endapo mmoja wetu ataanguka. Mchezo tuliokuwa tukiupenda sana ulikuwa mpira wenyewe tukiita”chandimu” Mtaa wetu ulikuwa unaitwa Kipata Street. Jina hili wengu hawalijui asili yake lakini ni moja ya vijiji ambavyo “mvumbuzi” David Livingstone alivipitia katika safari zake Nyasaland.

Mtaa wa mbele ya Kipata ni mtaa maarufu wa Kitchwele Street sasa unaitwa Mtaa wa Uhuru. Hakuna ajuaye hili neno “Kitchwele” nini maana yake. 

Lakini mtaa huu umepata heshima kubwa kwa kubadilishwa jina na kuitwa “Uhuru” Tanganyika ilipojikomboa kutoka ukoloni wa Waingereza tarehe 9 Desemba 1961. Nyuma wa Kipata Street ulikuwa mtaa wa Kirk Street sasa unaitwa Mtaa wa Lindi. Asili ya jina la Kirk ni Consular John Kirk aliyekuwa akitazama maslahi ya Waingereza Zanzibar. Sasa wazee wetu walikuwa hawawezi kulitamka jina hilo kama litakiwavyo badala yake wakawa 

wanasema “Kiriki” jina lililodumu hadi mtaa ulipobadilishwa jina. Nakimkumbuka kibao chake cha mtaa kiliandikwa kwa wino mweupe kwenye kibao cheusi “Kirk Street.” Nyuma ya Kirk Street ulikuwa mtaa wa Somali na nyuma ya Somali kulikuwa “Kiungani Street.” Asili ya jina hili ni Kiungani Zanzibar ambako Universities’ Mission to Central Africa (UMCA) ilijenga kanisa lake la kwanza pwani ya Afrika Mashariki katika miaka 1800.

Sasa tuingie katika mitaa ya kukatisha. New Street ndiyo ilikuwa inatengeanisha Gerezani na Uwanja wa Mnazi Mmoja, kisha inafuatia mtaa wa Livingstone, Sikukuu, Swahili, Nyamwezi, Congo na mwisho Msimbazi. Kisha kulikuwa na mitaa miwili midogo, Somali Kipande na Mbaruku. Kwa wakati ule kwa ajili ya udogo wangu ilikuwa shida sana kupambanua kuwa majina ya mitaa hiyo ya Kipata, Kirk, Livingstone na Kiungani ilikuwa ni kiashiria kuwa Tanganyika ilikuwa chini ya ukoloni wa Waingereza. Kwa Waingereza majina hayo yalikuwa yanawakumbusha mashujaa wao akina David Livingstone, Morton Stanley na ushawishi wao katika sehemu ambazo Waingereza walituma watu wao ama kuja “kuzivumbua” au kutawala. Juu ya hayo Gerezani ilijipambanua na mitaa mingine ya Dar es Salaam kwa kuwa na wapigania uhuru wengi waliokuja kutoa mchango mkubwa katika TANU. 

Lakini kwa bahati mbaya sana kwa hao wazalendo wote mchango wao haujathaminiwa wala hakuna leo mtu anaewafahamu au kuwakumbuka. Sasa hebu tuanze matembezi ya nyumba kwa nyumba kuzipitia nyumba walokuwa wakiishi wazalendo wapigania uhuru wa Tanganyika ili tuweakumbuke na tueleze yale waliyofanya wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Sasa hebu tuanze Kipata Street inapoanza Gerezani. Kipata Street inaanzia kule Msimbazi.Pale kulikuwa na nyumba ya Abdallah Salum Matimbwa akifanya kazi Relwe. Nyumba yenyewe ya asili leo haipo. Mtoto wa Mzee Abdallah Salum Matimbwa, Salum Matimbwa amejenga ghorofa. TANU ilipoanzishwa Abdallah Salum Matimbwa alikuwa mmoja wa wanachama wake wa mwanzo mwanzo lakini kwa kuwa wakati ule kudai uhuru lilikuwa jambo la hatari na yeye alikuwa mwajiriwa alijiunga TANU na kuwa mwanachama kwa siri. Halikadhalika alikuwa mwanachama wa Zaramo Union chama cha kikabila kikiendeshwa na Max Mbwana. Vyama hivi vya kikabila Waingereza wakivipenda sana kwa kuwa viliwasaidia katika ile njama yao wa “wabague uwatawale” Salum Matimbwa anaingia katika historia ya ukombozi wa Tanganyika si tu kama mwanachawa wa awali waliojiunga na TANU kabla ya 1958 bali kama mmoja wa wazalendo waliochanga fedha kuanzisha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Fikra ya kuanzisha Chuo Kikuu inasemekana ilianza na Nyerere akiwa na Dossa.

Ilkuwa kawaida ya Dossa baada ya mikutano ya TANU pale Mnazi Mmoja kumchukua Nyerere na gari lake kumrudisha Pugu. Njia ya zamani kwenda Pugu ilikuwa inapita hapo kilipo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Sasa ilikuwa kiza kimeingia na walitaka kutoka nje ya gari kuangalia mandhari ya Dar es Salaam maana kutokea pale mji ulikuwa unapendeza sana kwa taa zilizokuwa zikiwaka barabarani. Nyerere alimwambia Dossa, “Dossa tukipata uhuru wetu hapa lazima tujenge Chuo Kikuu.” Hili wazo lilifanyiwa kazi na wananchi wakahamasishwa kuchangia ujenzi wa Chuo hicho. Fedha zilichangwa na Chuo Kikajengwa pale New Street kwenye kiwanja cha John Rupia alichokitoa kuwapa TANU. Hapo ndipo kilipoanza Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Abdallah Salum alikuwa mmoja wa wachangiaji wa chuo hicho na mwanae Salum Matimbwa hadi leo amehifadhi stakabadhi ya malipo ya sh. 50.00 stakabadhi ambayo ina saini ya Joseph Nyerere. Wazee hawa walikuwa wazalendo wa kweli kabisa. Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 na zilipokuwa zikianzishwa harakati za ushirika Abdallah Salum Matimbwa alitoa lori lake Commer Fargo DSY 435 kama mtaji kuingiza katika Coast Region Transport Company (CORETCO). Pamojanae katika kuanzisha CORETCO walikuwa wazee wengine kama Sharia Bofu na nduguye Ibrahim Bofu, Salum Kambi, Juma Mzee na wengineo.

Unateremka sasa Kipata unaelekea Mnazi Mmoja. Kipata kona na Congo kulikuwa na nyumba ya Ibrahim Hamisi mmoja wa waasisi wa African Association mwaka 1929. Huyu alikuwa Mnubi kutoka Darfur. Baba yake alikuwa askari wa Kinubi walokuja Tanganyika na Kamanda wa Kijerumani Von Wissman kuja kuwasaidia Wajerumani katika vita yao dhidi ya wazalendo wa Tanganyika akina Bushiri bin Harith wa Pangani na Chifu Mkwawa kutoka Kalenga. Ibrahim Hamisi akifanya kazi Government Press kama “composer.” Wajerumani walikuwa wajanja na wepesi katika kulipa fadhila. 

Waliwasomesha vizuri sana watoto wa askari wao waliowaleta Tanganyika kuja kuwasaidia kutawala. Kwa njia hii waliweza kujenga tabaka la wageni lililokuwa juu kupita wenyeji wa Dar es Salaam, Wazaramo, Wamashomvi nk. Hali hii kwa kiasi Fulani ilileta migogoro baina Wamanyema, Wazulu na Wanubi kwa upande mmoja ambao walionekana kama “watu wa kuja” na wenyeji wazawa wa Dar es Salaam kwa upande mwingine.

Kwa wakati ule kazi ya “composer” ilikuwa kazi yenye hadhi kwa Mwafrika na ilihitaji mtu aliyesoma. Ibrahim Hamisi alikuwa mmoja wa waasisi wa Al Jamiatul Islamiyya fiy Tanganyika chama cha Waislam kilichoanzishwa mwaka 1933 na kikajenga shule Al Jamiatul School New Street kona na Stanley Street ambayo jengo lake lipo hadi leo Mtaa wa Lumumba na Max Mbwana. Uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya ndani yake mlikuwa na Waarabu, Wanubi, 

Wazulu, Wamanyema, Wazaramo na makabila mengine ya pwani na mara nyingi Wazulu na Wanubi ndiyo wakishika uongozi. Na hii ilipata kujaleta mgogoro mkubwa mwaka 1940 kiasi cha kufunga shule na kwa muda hadi Gavana akaingia kati kusuluhisha. Hii Ilikuwa katika Ali Aljamiatul Islamiyya lakini hata katika African Association mambo yalikuwa hivyo hivyo. Mwaka wa 1933 kulitokea ugomvi uliosababisha secretary Kleist Sykes asuse chama hadi alipoombwa na Mzee bin Sudi aliyekuwa president ndipo aliporejea tena katika chama. Mzee Bin Sudi alikuwa Mmanyema. Hizi ndizo zililiwa siasa za wakati ule.

Mbele ya Kipata Street ukishapita Swahili Street unafika nyumba ya Hassan Machakaomo. Kizazi kingine cha wageni kutoka nje ya mipaka ya Tanganyika. Hassan Machakaomo ni mtoto wa Machakaomo Mzulu askari mamluki kama walivyokuwa Wanubi. Wazee wake waliletwa Tanganyika na Von Wissman kuja kuwasaidia Wajerumani kupigana vita dhidi ya wazalendo wa Tangnayika waliokuwa wanapinga utawala wa Wajerumani. Hassan Machakaomo alijulikana zaidi kama kiongozi wa Young Africans Football Club katika miaka ya 1950 na harakati za kudai uhuru zilipoanza mwaka 1954 Young Africans, “Yanga” kama ilivyokuwa inajulikana ilijinasibisha moja kwa moja na bila ya kificho na TANU. Si mbali na nyumba hiyo kwa mkono wa kulia Kipata kona na Sikukuu ilikuwa nyumba ya Clement Mohamed Mtamila ambaye katika miaka ya mwisho ya 1940 ndiye alikuwa katibu wa TAA baada ya African Association kubadilisha jina na kuitwa TAA. Hapa itabidi tusimame kidogo.


Kushoto ni Ally Sykes akiwa na miaka 17 na kaka yake Abdulwahid miaka 19 wakiwa katika unifomu za King's African Rifles (KAR) katika kikosi cha Burma Infantry Vita Kuu ya Pili1938 - 1945

Baada ya vita ya pili ya dunia vijana askari waliokuwa katika King’s Africa Rifles (KAR) 6th Batallion waliopigana Burma katika wengi wao wakiwa Dar es Salaam walianza kuwachachafya viongozi wazee waliokuwa wakiongoza TAA. Rais wa TAA wakati ule alikuwa Mwalimu Thomas Plantan mtoto wa Afande Plantan mkubwa wa askari mamluki wa Kizulu aliokuja Tanganyika na Von Wissman. Afendi Plantan alikuwa ndiye kiongozi wa askari wa Kizulu na mkubwa wa Wazulu wote pale mjini. Afendi Plantan hakutoroka na Von Wissman kurudi kwao Mozambique baada ya Vita ya Kwanza kumalizika na jeshi la Wajerumani kushindwa wakawa sasa wanatoroka kukimbilia Mozambique kupata hifadhi. Afande Plantan alibaki Dar es Salaam na kuweka makazi yake Mtaa wa Masasi Mission Quarter.

Mtoto wa Affendi Plantan Thomas, akijulikana kwa jina lingine la Sauti alipata elimu nzuri katika shule ya Kijerumani akawa mwalimu wa shule. 

Thomas Plantan alistawi hadi kufikia kushika uongozi wa African Association. Sababu ya uongozi huu wa wazee kuchachafwa ni kuwa vijana walikuwa wakiona chama hakina malengo ya kudai uhuru wa Tanganyika. Kwa hakika chama kilikuwa kimezorota sana. Mikutano ilikuwa haiitishwi na chama kilikuwa hakina fedha za kuweza kujiendesha. Hapa ndipo tunakutana na kijana Abdulwahid Sykes, mtoto wa Kleist Sykes, (Mzulu mwingine) yeye na kundi la vijana wenzake, Dossa Aziz, Hamza Mwapachu, Stephen Mhando, Dr Vedasto Kyaruzi wakawa wanatafuta njia za kuingia katika uongozi wa TAA. Tatizo lililowakabili ikawa wazee hawataki kuachia hatamu za uongozi wala kuitisha mkutano wa uchaguzi.

Thomas Plantan alikuwa muwindaji na alitumia muda wake mwingi porini kuwinda, hakuwa na muda na siasa za mjini. Hata miaka mingi baada ya kifo chake, bado kuta za nyumba yake Masasi Street, Mission Quarter zilipambwa na vichwa vya pofu na mbogo aliowaua porini. Hata hivyo walikuwapo wazee ambao ingawa walikuwa watu wazima lakini walikuwa wanataka kuona mabadiliko katika TAA. Mmoja wa wazee hawa alikuwa Schneider Plantan, mdogo wake Thomas Plantan. Katika mkutano ulikoitishwa Arnautoglo Hall mwaka 1950, Schneider alifanya vurugu mbele ya maofisa wa kikoloni kiasi ilibidi wazee wakubali kuitisha mkutano wa uchaguzi, lakini kabla ya uchaguzi kufanyika Abdulwahid Sykes na Hamza Mwapachu walivamia ofisi za TAA pale New Street na kuchukua uongozi kwa nguvu wakaitisha mkutano wa uchaguzi na Dr Vedasto Kyaruzi akachaguliwa President na Abdulwahid Sykes Secretary. Hii ilikuwa mwaka 1950.

Inasemekana harakati za kupanga mipango ya kufanya mapinduzi katika TAA ilikuwa ikipangwa Ilala Welfare Centre ambako Hamza Mwapachu alikuwa akifanya kazi kama Welfare Officer, mahali pengine ilikuwa Kariakoo Market ambako Abdulwaihd alikuwa Market Master. Tuachie hapa, tutakuja kuyazungumza haya huko mbele. Turudi kwenye nyumba ya Mzee Mtamila. Nyumba hii leo haipo, ilipokuwa nyumba ya Mzee Mtamila kuna gorofa na si watu wengi wanofahamu historia iliyopata kubebwa na nyumba ile. Ilikuwa katika nyumba ile ndipo Julius Nyerere aliposhauriwa na Halmashauri Kuu ya TANU chini ya uenyekiti wa Mzee Mtamila ajiuzulu ualimu aiendeshe TANU. Hii ilikuwa baada ya Nyerere kurejea kutoka Umoja wa Mataifa mwaka 1954 na wakoloni wakaona jinsi TANU ilivyokuwa ikipata nguvu siku hadi siku. Mmoja wa viongozi katika Halmashauri hii ya TANU ya 1955 waliomshauri Nyerere aache kazi ya ualimu aendeshe TANU alikuwa Tatu bint Mzee na Idi Faizi Mafongo. Mafongo ndiye alikuwa mweka hazina wa Al Jamiatul Islamiyya na mweka hazina wa TANU vilevile. Leo hakuna anaewajua watu hawa wala historia haiwataji lakini walifanya kazi kubwa sana. Iddi Faizi Mafongo ndiye aliyefanikisha ukusanyaji wa fedha za TANU ziliotumiwa kumpeleka Nyerere Umoja wa Mataifa, New York na alichota fedha nyingine katika hazina ya Aljamitul Islamiyya kutunisha mfuko wa TANU.

Hili la kuchota fedha za Al Jamiatul Islamiyya halikuwa na shida yoyote kwani katibu wake alikuwa Ali Mwinyi Tambwe mmoja wa watu wa mwanzo kujiunga na TANU. (Tutaona huko mbele Ali Mwinyi Tambwe aliingia vipi TANU na mchango wake katika kuiangusha serikali ya Zanzibar mwaka 1964 jambo lilikuja kumtia simanzi na huzuni kubwa kwa yale yaliyokuja kutokea – mauaji yaliyokuwa hayana sababu na maonezi ya kipuuzi kabisa). Licha ya hilo Abdulwahid na Ally walikuwa na sauti katika jumuia hiyo kwa kuwa ilianzishwa na baba yao na walisoma Al Jamiatul Islamiyya Muslim School.

Tatu bint Mzee, Bi Hawa Maftah, Bi Titi Mohamed, Mwalimu Sakina Arab na  wanawake wengine wa mjini ndiyo waliotia nyimbo za Lelemama katika kwaya ya TANU nyimbo ambazo zilihamasisha watu kupita maelezo. Kuna nyimbo moja ilikuwa inaimbwa hivi:

“Muheshiwa nakumpenda sana,
Wallahi sina mwinginewe,
Insha Allah Mungu yupo,
Tanganyika tutajitawala”

Hii ndiyo ilikuwa nyimbo ya mwanzo ya lelemama kutiwa katika harakati za kudai uhuru na baada ya hapo zikaja nyingine nyingi lakini maarufu na inayofahamiza zaidi ni “Hongera Mwanangu.” Mzee Mtamila ameacha hazina kubwa sana ya picha za siku za mwanzo za harakati za kudai uhuru zikionyesha wana TANU katika mikutano ya mwanzo Mnazi Mmoja. Inaaminika picha hizi zilipigwa na Mzee Shebe ambae studio yake ilikuwa Livingstone Street si mbali na nyumbani kwa Mzee Mtamila. Baadhi ya picha zikimuonyesha Mzee Mtamila, Bibi Titi Mohamed, John Rupia wakiwa wamekaa katika jukwaa huku Mwalimu Nyerere akihutubia wananchi.

Ukivuka Kipata mbele unakutana na Livingstone Street, ukitazama mkono wa kulia kabla ya kufika New Street labda nyumba tatu kabla pale ndipo ilipokuwa nyumba ya Kleist Sykes, Mtoto wa Sykes Mbuwane, askari wa Kizulu aliyekufamaji Mto Ruaha akiwa anarudi vitani baada ya kumshinda Mkwawa. Hii ilikuwa mwaka wa 1898. Kuna kisa kitatokea miaka 56 baadae kati ya kizazi cha Mtwa Mkwawa na Sykes Mbuwane. Wajukuu wao watakuwa wamoja katika TANU kupambana na ukoloni. Nitakieleza kisa hicho kwa ufupi.

Mwaka 1954 fuvu la Mkwawa liliporudishwa Kalenga Adam Sapi Mkwawa mjukuu wa Mtwa Mkwawa aliwaalika Abdulwahid Sykes mjukuu wa Sykes Mbuwane, adui wa babu yake na Dossa Aziz kuja katika sherehe ya kupokea fuvu lile. Ilikuwa pale Kalenga ndipo Abdulwahid alipomuingiza Adam Sapi katika TANU kwa siri na kumfanya awe mmoja wa machifu wa mwanzo kabisa kuiunga mkono TANU. Wakati Chifu Adam Sapi anajiunga na TANU chama kilikuwa hakijamaliza hata mwezi moja katika uhai wake. Tutazieleza habari za Abdulwahid Sykes na ushawishi mkubwa aliokuwa nao katika TAA na baadae TANU na katika wanasiasa wa wakati ule pamoja na machifu tutakapofika kusanifu makazi yake pale Stanley Street kona na Sikukuu Street. (Baada ya uhuru mtaa huu ulikuja ulibadilishwa jina na kuitwa Aggrey) Ila ieleweke tu kuwa kwa wakati ule wa siku za mwanzo za harakati kuanzia enzi za TAA baadhi ya machifu hawakuitazama TAA na baadae TANU kwa jicho zuri sana. Hofu kuu na ndiyo hofu aliyokuwanayo mshirika wao Muingereza katika ule mfumo “indirect rule” wa Lord Lugard ni kuwa TANU imekuja kuwanyang’anya madaraka yao.

Sasa turejee kwenye nyumba ya Kleist Sykes hapo Kipata. Kwa hakika Kleist alikuwa mtu wa mipango na mjengaji wa mikakati si tu katika maisha yake binafsi bali hata katika kupeleka mbele maslahi ya Waafrika katika Tanganyika. Kleist alizaliwa Pangani mwaka 1894. Akiwa na umri mdogo wa miaka 25 alikuwa keshaasisi African Association  mwaka 1929 na kufikia mwaka 1933 aliasisi Al Jamiatul Islamiyya Fiy Tanganyika, hicho ni Kiarabu (maana yake kwa Kiswahili ni “Umoja wa Waislam wa Tanganyika”). Mwaka wa 1924 Dr Aggrey alikuja Tanganyika kama mjumbe katika kamisheni moja ya elimu kuchunguza hali ya elimu kwa Waafrika wa Tanganyika. Kwa wakati ule Dr Aggrey alikuwa mfano wa Mwafrika aliyeelimika sana. 

Alipokuwa Dar es Salaam Dr Aggrey alikutana na Kleist na katika mazungumzo Dr Aggrey alimshauri Kleist kuwa endapo Waafrika wanataka kupiga hatua ni lazima waunde umoja wao. Ilimchukua Kleist miaka mitano hadi kuja kufanikisha ushauri ule na kuunda African Association akiwa katibu muasisi.

African Association na Al JAmitul Islamiyya ndivyo vilivyokuja kuwa chimbuko la kuundwa kwa TANU kwa kutoa viongozi kama Abdulwahid na Ally Sykes, Ally Mwinyi Tambwe, Iddi Faizi Mafongo, Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Abdalla Iddi Chaurembo, Sheikh Suleiman Takadir na wengineo na wanachama wake wa mwanzo. Kleist alilelewa nyumba moja na Thomas, Schneider na Mashado Plantan baada ya kifo cha baba yake. Hapa ningependa kidogo kuwaeleza wasomaji asili ya majina haya ya Kikristo na yenye asili ya Kijerumani. Hawa watoto baba zao walikuwa askari katika jeshi la Wajerumani. Wajerumani baada ya kuituliza Tanganyika kwa mtutu wakaliita lile jeshi lao la mamluki wa Kinubi na Wazulu “Germany Constabulary.” Mkubwa wa jeshi hili alikuwa Afendi Plantan, baba yao Thomas, Schneider na Mashado.

Sasa inasemekana wakizaliwa watoto Wajerumani ndiyo walikuwa wakitoa majina kwa watoto hao na majina waliyowapa ni ya Kijerumani ndiyo kukawa na Kleist, Thomas, Schneider, Mashado na mengineyo. Lakini wakiondoka tu palepale baba zao wakawa wanatoa majina ya Kiislam kwa kuwa wao walikuwa Waislam hawakupenda sana watoto wao wajulikane kwa majina ya Kikristo. Kwa mfano Kleist jina lake ni Abdallah, Shneider jina lake ni Abdillah na Mashado jina lake ni Ramadhani. Hadi leo kwenye kaburi la Kleist pale Makaburi ya Kisutu jina lake limeandikwa: “Kleist Abdallah Sykes.” Haieleweki kwa nini yeye hakupenda kujinasibu na jina lake la asili “Mbuwane” au “Abdallah” na kwa nini watoto wa Plantan kwa jina lao la asili la “Mohosh” ambae huko kwao Kwalikunyi Mozambique alikuwa chifu wa Kizulu.  Sasa zaidi ya miaka mia moja ukoo wa Sykes umevuma na kujulikana katika siasa na biashara kwa jina hilo la Kijerumani na hadi leo ukoo wa Plantan ambao uko Mission Quarter, Mtaa wa Masasi ni katika koo maarufu sana Dar es Salaam nao wanajulikana kama akina Plantan.

Kleist alisoma shule ya Kijerumani na shule yenyewe ndiyo hii sasa Ocean Road Hospital. Alisoma hadi darasa la sita na alipomaliza shule hapo alikuwa anasema Kijerumani, anajua short hand (hati mkato) na kupiga taipu. Huu ulikuwa ujuzi mkubwa sana kwa Mwafrika kuwa nao wakati ule. 

Lakini alipomaliza shule Wajerumani hawakumwacha afanye kazi ofisini walimtia katika jeshi na Vita Vya Kwanza vilipoanza mwaka 1914 Kleist na ndugu yake Scheneider Plantan walijikuta wakielekea Tanga kupambana na majeshi ya Kiingereza. Mkuu wa majeshi ya Kijerumani alikuwa Von Lettow Voberk na Kleist ndiye alikuwa Aide De Camp wake. Cheo kizito sana wakati ule kwa Mwafrika kukibeba. Baada ya vita na kushindwa kwa Wajerumani baadhi ya askari wa Kizulu walikimbia na kamanda wao Vorbeck na kuingia Mozambique. Wazulu waliobaki Tanganyika walikuwa wamepwelewa.  

Kleist alikuwa mateka wa vita na alipoachiwa alianza kujifunza Kiingereza na hakutaka tena kujiunga na jeshi. Habari za Kleist ni nyingi sana na mengi katika maisha yake aliandika kwa mkono wake mwenyewe. Mwaka 1969 mjukuu wake, Daisy Sykes Buruku kwa msaada wa msaada wa baba yake, Abdulwahid Sykes na akiwa chini ya Profesa John Illife wa Chuo Kikuu Cha Cambridge wakati ule, Iliffe akisomesha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Disy akiwa mwanafunzi wake alikuja kuandika upya maisha ya babu yake “Kleist Sykes The Townsman” katika kitabu “Modern Tanzanians” kilicho haririwa na John Illife. Katika kitabu hicho Kleist anatoka kama mwanasiasa makini na muasisi wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. 

Kleist alifanya mengi Dar es Salaam, alijenga shule Al JAmiatul Muslim School, jengo la TAA ambamo TANU ilikuja asisiwa mwaka 1954, alikuwa katika baraza la Munispal Council, memba wa Dar es Salaam Maulid Committee,  alikuwa kiongozi wa chama cha Wafanyakazi wa Relwe, alikuwa mfanya biashara mkubwa na mwanachama wa Chamber of Commerce Mwafrika pekee katika chamber.

Kleist aliwanunulia vyombo vya muziki wanae wakati huo vijana wadogo baada ya Abdulwahid na Ally kurudi vitani Burma mwaka 1945 walipokwenda kupigana kama askari katika KAR. Wanae pamoja na vijana wenzao wa mjini kama Matesa, Said Kastiko, Msikinya (huyu alikuwa ametokea Afrika ya Kusini), Dome Okochi Budohi na nduguye akiitwa Martin (hawa walikuwa wanatoka Kenya) wote hawa wakaanzisha bendi iliyojulikana kama "Skylarks." Baadae walibadili jina na kujiita "The Blackbirds" Kleist mwenyewe akiwa patron wa bendi na akihudhuria maonyesho ya bendi hiyo. 

Kulikuwa na bendi kama hiyo siku zile Johannesburg ikiitwa “Skylarks.” Hili ni kundi ambalo Miriam Makeba wakati huo msichana mdogo alikuwa akiimba. Bendi hii ikaja tena baadae kubadili jina na kuitwa “Merry Makers.” Bendi hii ilipendwa sana na vijana wa mjini wa wakati ule hasa kwa kuwa wao walipiga ile mitindo ya Ulaya kama Waltz, Foxtrot, Quick Step nk. Bendi hii ikipiga nyimbo zilizokuwa maarufu wakati ule wa vita si Tanganyika tu bali hata Ulaya kama “More,” Chacanuga Chouchou,” “Siboney,” “Siboney,” “Fly Me to The Moon,” “Perfidia” na nyinginezo, nyimbo ambazo zilipewa umaarufu na wanamuziki wakubwa wa Amerika na Uingereza kama Glenn Miller, Louis Armstrong, Charlie Parker, Benny Goodman, Andrew Sisters na wengineo.

Merry Black Birds - Kushoto: Wa Pili ni Ahmed Rashad Ali, Ally Sykes, Matesa Kushoto: Waliosimama Nyuma Wa Pili Abbas Sykes

Vijana hawa walikuwa wakipendwa sana hata Zanzibar ambako wakipiga Victoria Garden na kule mashabiki wao walikuwa akina Ahmed Rashad Ali (huyu alikujakuwa mtangazaji maarufu sana na mwanapropaganda mahiri katika Radio Afrika Huru kutoka Cairo wakati wa kupigania uhuru) nduguye Prince Sudi, Abdillah Masud maarufu kwa jina la “Smuts,” (huyu alikuwa vitani Burma pamoja na akina Sykes), Mkubwa Mohamed Mashangama maarufu kama “Bwana Mkubwa Shoto” (jina hili la “Shoto” alilipata kwa kuwa alikua mcheza mpira maarufu na akipiga mashuti makali kwa mguu wake wa kushoto),  na jamaa wengi. Kleist  alipenda kukaa meza ya pembeni pale Arnatuoglo Hall nadhifu katika suti yake akitingisha mguu sawa na midundo iliyokuwa ikiporomoshwa na watoto wake na rafiki zao, picha ya King George ikiwa inamkodolea macho kwa juu ilipokuwa imetundikwa katika ukumbi ule. Baada ya kifo cha King George, ikatundikwa picha ya Queen Elizabeth ambayo hata sisi tuliikuta pale Arnautoglo katika miaka ya 1950 mwishoni. Hebu tusimame kidogo hapa.

Vijana hawa walipotoka utotoni na kuwa watu wazima na wakaanza siasa misingi hii waiyoijenga katika urafiki wao wa utotoni uliwasaidia sana katika harakati. Aman Thani mmoja wa viogozi wa Hizbu au (Zanzibar Nationalist Party) anasema ilikuwa Abdulwahid Sykes na Dossa Aziz ndiyo walikuja na Nyerere Zanzibar kumjulisha kwa Karume. Historia bado haijaweka wazi mchango wa hawa watu watatu katika kuundwa kwa Afro-Shirazi Party lakini Issa Nassoro Ismaily amepata kusema kuwa Abdulwahid alipata kumweleza masikitiko yake kwa yale yalipotokea Zanzibar baada ya mapinduzi na akasema kuwa hapendi yeye kuzungumza suala lile kwa kuwa anahisi litavunja udugu baina yao. Halikadhalika Ali Mwinyi Tambwe hakupenda kabisa anasibishwa na mapinduzi yaliyotokea Zanzibar lau kama yeye alikuwa mmoja wa watu wa ndani katika kupanga mipango ile. Tuendelee.

Leo hii ukiangalia picha za wakati ule za bendi hii jinsi walivyokuwa wamevaa suti zao na “bow - tie” na ukiangalia zile ala za muziki pamoja na piano unaweza ukakosea ukadhani hiyo ni bendi ya Count Bessy, Louis Armstrong au Charlie Parker wa Marekani. (Kipindi hiki kiliibua vipaji, Hamza Aziz, mtoto wa Aziz Ally mmoja wa matajiri wakubwa Waafrika Dar es Salaam na rafiki wa Kleist alikuwa akiimba nyimbo za Nat King Cole na yeye mwenyewe alikuwa akijiita Nat King Cole). Harakati za kudai uhuru zilipoanza mwaka 1954 Hamza Aziz alikuwa katika jeshi la polisi la kikoloni na kaka yake Dossa Aziz alikuwa mstari wa mbele na Nyerere katika TANU. Inasemekana TANU wakimtumia sana Hamza kupata siri za wakoloni.  Sasa njoo angalia picha za mama zetu na mitindo ya nywele na magauni waliyovaa na mikanda mipana mithili ya wanawake wa Kizungu. Hapo wapo Arnatouglo Hall wakicheza mziki wa The Skylarks. Mama zetu waliokuwa ehe kidogo walikuwa wanavaa na glovu nyeupe kama wanawake waKizungu.

Nikiwa mtoto mdogo sana nina kumbukumbu ya party moja nyumbani kwetu Kipata Street na nyimbo ambazo zikipendwa sana wakati ule zilikuwa za Septet Habanero kutoka Cuba. Katika waliohudhuria party ile nina kumbukumbu ya Dome Okochi Budohi aliyekuja kuwa mmoja wa wanachama wa mwanzo wa TANU na mtu aliyekuwa inasemekana kiungo kati ya TAA na KAU ya Jomo Kenyatta. Okochi Budohi alikamatwa mara tu hali ya hatari ilipotangazwa Kenya baada ya mapambano kati ya Wakikuyu na Waingereza kupamba moto. Msako huu na kamata kamata ilokwenda pamojanayo ilipewa jina “Operation Anvil” na Waingereza. Kundi zima la viongozi wa Kenya kama Kenyatta, Bildad Kaggia, Paul Ngei, Kungu Karumba na wengine waliwekwa kizuizini sehemu moja Kenya ijulikanayo kama Manyati. Dar es Salaam Wakenya ambao walikuwa wanachama wa TAA nao walitiwa mbaroni na kurudishwa Kenya chini ya ulinzi mkali wakiwa wamefungwa minyororo.

Turejee kwa Kleist. Hapakuwa na mfano wa Kleist katika mji wa Dar es Salaam. Kleist alikuwa na kinyozi wake tena Muhindi akija mnyoa ndevu na nywele nyumbani. Kleist alikuwa anakwenda kazini kwa baskeli kitu nadra katika miaka ile na aliwanunulia wanae baskeli ndogo za kupanda kitu ambacho Mwafrika wa kawaida hakumudu. Kleist akiwashangaza wengi kwani alikuwa akila juu ya meza na wanae. Utamaduni wa wakati ule ulikuwa watu kula chini juu ya mkeka au jamvi. Wenzake wakimuona Kleist akiishi kama Mzungu. Vilevile wakati wote yeye alikuwa kavaa suti, hata anapokwenda msikiti kwake kusali pale Kipata. Msikiti huu upo hadi leo. Nyumba aliyoacha Kleist sasa haipo na mtoto wake, Ally Sykes amejenga nyumba ya gorofa tano pale. Nyumba hii ndimo alimozaliwa Ally na Abbas na ina historia kubwa kabisa kama ilivyokuwa historia za maisha ya wanae katika historia ya TANU na kudai uhuru wa Tanganyika. Hatuwezi kuelezana yote hapa.

Kleist alikuwa mtu maarufu akialikwa kwa Gavana Government House na akitakiwa ushauri katika mengi yaliyohusu siasa za mji wa Dar es Salaam katika miaka ya 1930 hadi alipofariki mwaka wa 1949. Kleist  alipata maziko makubwa hayajapata kuonekana Dar es Salaam ya wakati ule na kaburi lake hadi leo lipo pale Kisutu, pamoja na rafiki zake wengi aliokuwanao katika harakati za siasa za mji wa Dar es Salaam katika miaka ya 1940. 

Ukitembea tembea katika makaburi yale utaona kaburi la Ali Jumbe Kiro, Maalim Popo Saleh na wengineo, wenzake aliokuwanao katika African Association, Al Jamiatul Islamiyya na katika Dar es Salaam Maulid Committee.

Ila ikutoshe tu kuwa wakati mipango ya kuibadili TAA kuwa chama kamili cha siasa cha siasa wakati wa uongozi wa Dr Vedasto Kyaruzi na Abdulwahid na Ally Sykes, Ally alikuwa ameficha mashine ya kurudufisha katika nyumba hii ya baba yake akiandika makaratasi ya kuwataka Waafrika wa Tanganyika wajiunge TAA kwa wingi. Makaratasi haya ambayo Waingereza walikuwa wakiyaita ya “uchochezi” alikuwa akiyasambaza mjini kote na mengine akiwapa wafanyakazi katika treni wakiyamwaga njia nzima katika Reli ya Kati kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma na Mpanda. Makachero wa Special Branch, mmoja wapo aliyewashughulisha sana wazalendo akiwa Amiri Kweyamba wakawa wanataka kujua chanzo cha makaratasi yale. Huyu Kweyamba hata baada ya uhuru aliendelea kuwa katika Usalama wa Taifa. Hivi karibuni Waingereza wameziweka hadhir nyaraka zilizokuwa za siri na imekujafahamika kuwa walishamweka Abdulwahid Sykes katika uchunguzi wakati akiwa Market Master Kariakoo Market kwa ajili ya harakati zake za siasa katika TAA na baadae katika TANU. (Tutazizungumza harakati za Abdulwahid Sykes pale sokoni tukishaingia yaliyopitika mitaa ya Kariakoo harakati za kujenga TANU zilopoanza). Sasa hali kama ilikuwa hivyo ni wazi kuwa hata mdogo wake Ally walikuwa wamshemjaza katika darubini zao.

Siku moja ghafla Ally Sykes akiwa katika shughuli zake za kuyachapa makaratasi yake ya “uchochezi” akasikia mlango unagongwa. Kuchungulia anamuona Kweyamba kasimama mlangoni kwake kama jini kaja kutoa roho ya mtu. Haraka sana akarudi chumbani ikawa sasa yeye na mkewe Bi. Zainab wanahangaika kuyakusanya makaratasi kuyatia moto na mengine kutumbukiza chooni. Ally Sykes akikumbuka kisa hiki anasema alichukua karatasi moja na wino wake akalimeza. Katika vitu ambavyo Ally Sykes anasema vilimkera sana baada ya uhuru ni pale Nyerere alipompa kazi ile ile Kweyamba katika Tanganyika huru. Wakati wa kupigania uhuru Nyerere alikuwa hapungui nyumba hii. Hii nyumba ya Kipata ya Ally Sykes, nyumbani kwa Abdulwahid Sykes Stanley Street na Sikukuu na nyumbani kwa Dossa Aziz Mbaruku Street ndizo zilikuwa nyumba za Nyerere akiingia kwa mlango wa mbele akitokea mlango wa uani. Kwa hakika hizi nyumba zote zimehifadhi kumbukumbu, vituko, vichekeso na mengi sana ya Mwalimu Nyerere na TANU. Ni vigumu kueleza yote hapa. Moja ya kisa cha kusisimua na ambacho si wengi wanakifahamu ni kile cha Mzee Said Chamwenyewe. Nitakieleza kwa muhtasari.

Baada ya TANU kuasisiwa Nyerere alikwenda kwa Msajili wa Vyama kusajili TANU. Msajili alikataa kuisajili TANU kwa kisingizio kuwa TANU ilikuwa haina wanachama. Nyerere alitoka kwa msajili akaja hadi Kipata nyumbani kwa Ally Sykes kuja kutoa taarifa. Abdulwahid na Ally walikuwa wakimsubiri. Bi Zainab mkewe Ally Sykes anasema Nyerere alipofika alikaa kwenye sofa na kujiinamia kwa huzuni. Wenzake walikuwa kimya wakimsubiri atoe taarifa. Alipoeleza kuwa TANU imekataliwa, Abdulwahid palepale alitoa amri atafutwe Said Chamwenyewe. Alipofika Chamwenyewe Abdulwahid alimwambia Chamwenyewe aende Rufiji akaitafitie TANU wanachama ile chama kipate usajili. Chamwenyewe alikuwa anatoka Rufiji. Mzee Chamwenyewe mchango wake ingawa haujulikani lakini alifanya mengi katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Yeye alikuwa anakwenda Rufiji kwa baiskeli na katika vijiji alivokuwa akipita alikuwa akihamasisha watu kujiunga na TANU na akiwauzia kadi. Ilikuwa baada ya Chamwenyewe kurejea kutoka Rufiji na kumkabidhi Abdulwahid rejests ya wanachama wa TANU Rufiji ndipo TANU ilipopewa usajili kwa shingo upande na Waingereza. Mzee Chamwenyewe hakuwa mgeni katika siasa za kudai uhuru wa Tangnayika. Alikuwa mmoja wa wanachama shupavu wa TAA na Agosti 1954 Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulipokuja Tanganyika kukagua hali ya siasa Said Chamwenyewe ndiye aliyekuwa msemaji mkuu kwa niaba ya TANU, pamojanae wajumbe wengine walikuwa Sheikh Suleiman Takadir, Mohamed Jumbe Tambaza, Clement Mtamila na wazee wengine. Hawa walikuja kuunda Baraza la Wazee wa TANU mwaka 1955 baada ua kuundwa kwa chama hicho.

Ally Sykes amekaa kitako na akishirikiana na mwandishi ameandika kumbukumbu zake. Awali mswada ulipelekwa kwa wachapishaji kwa jina la “Under the Shadow of British Colonialism The Life of Ally Kleist Sykes” lakini wachapishaji baada ya kuupitia mswada wamesema kitabu kiitwe “Broken Dreams The Life of Ally Sykes” na sababu walizotoa ni kuwa yale alotegemea Ally Sykes angeyaona katika Tanganyika huru yalikwenda kinyume na matarajio yake. Mojawapo kubwa ni kuwa hadi sasa anafikia umri mpevu kabisa na kaka yake kuwa marehemu miaka mingi na kuwa baba yao alijitolea kwa hali na mali katika kuipiganiaTanganyika mchango wa ukoo wake haujathaminiwa. Historia ya uhuru ikitajwa inaanza na jina la Nyerere peke yake. 

Inasikitisha sana kuwa jumba lile ilipoasisiwa TANU ambalo lilijengwa na Kleist Sykes, Mzee bin Sudi na wazee wengine hakuna hata kumbukumbu yao.

Ikitazamana na nyumba ya Kleist ndipo alipokuwa akiishi Salum Abdallah Muyukwa Samitungo Mwekapopo wa kabila la Wamanyema, yeye alizaliwa katika boma la Wajerumani Shirati. Baba yake alikuja Tanganyika kama askari katika jeshi la Kijerumani mwishoni mwa miaka ya 1800. Yeye alikuwa na nyumba yake Mbaruku Street lakini aliona bora apange nyumba pale Kipata kwa kuwa pale ndipo barza yake ilipokuwa ingawa Mbaruku na Kipata si mbali lakini kwa wakati ule palionekana pembezoni. Nyumba hii alopanga babu yangu ilikuwa mali ya Abdallah Simba, aliyekuwa liwali Songea. 

Abdallah Simba alikuwa akiishi Songea na ukoo wake ni katika koo mashuhuri kule Songea. Nikiwa mtoto namkumbuka sana huyu mzee akija Dar es Salaam na Landrover yake mwenyewe na siku zote akivaa kanzu nyeupe na koti. Huyu mzee alikuwa mtu wa kujiweza sana na alikuwa na nyumba nyingine Somali Street akiishi bint yake Bi Habiba. Huyu bi mkubwa bado yu hai na naamini ni hazina ya kumbukumbu. Huyu mama naamini ni katika akina mama Waswahili manesi wa mwanzo kabisa Tanganyika.

Abdallah Simba alikuwa rafiki mkubwa wa Salum Abdallah. Halikadhalika Kleist Sykes na Salum Abdallah licha ya kuwa walikuwa majirani, walikuwa 

wakifanya kazi pamoja katika Tanganyika Railway na wake zao Bi Mluguru bint Mussa, mke wa Kleist na Bi Zena bint Farijala walikuwa mashoga. 

Ushoga mkubwa kabisa wa kufuliana vidani vya dhahabu. Mabibi hawa bila ya kujua athari za ushoga wao wamekuja kuwa hazina kubwa sana kuhusu maisha ya waume zao na katika kueleza maisha hayo leo tumekuja kufahamu mengi kuhusu maisha ya watu wa Dar es Salaam na nyakati zao. Bi Zena juu ya umri mkubwa alokuwa nao alikuwa mpenzi wa Harry Belafonte na kila alipopata nafasi alipenda kuieleza senema ile kwa wajuu zake (mmoja wapo akiwa mwandishi) alocheza Belafonte iitwayo “Island in the Sun.” Senema hii ilikuja Tanganyika katika miaka ya mwisho ya 1950 na ilisisimua wengi kwanza kwa haiba ya Belafonte mwenyewe na nyimbo aloimba katika senema ile. Lakini kubwa zaidi ambalo nahisi Waafrika wengi walotazama senema ile lililowaathiri ni ile hadith yenyewe, maana ilikuwa inahusu mapambano kati aya Waafrika na ukoloni wa Muingereza. Vilevile kulikuwa na kisa cha mapenzi kati ya Harry Belafonte aliyekuwa nyota wa mchezo ule na msichana wa Kizungu. Kilichomfurahisha sana Bi Zena ni kule yule yule msichana wa Kizungu kukataliwa na mtu mweusi, Belafonte. Wakati ule Belafonte ndiyo alikuwa anainukia na nyimbo zake kama “Round the Bay of Mexico,” “Banana Boat,” “Jamaica Farewell” na nyimbo nyingine zilikuwa zikisikika katia radio kila siku. Biti Farijala kama alivyokuwa Biti Mluguru, waume zao ndani ya nafsi zao walichukia kutawaliwa na huenda katika mazungumzo yao ya faragha hili lilijitokeza mara kwa mara. Hali ya wakati ule haikuruhusu Waafrika kudai waziwazi haki yao ya kujitawala lakini mambo yalipowiva wazalendo wa Tanganyika hawakusita kumuomba Muingereza kufunga virago na kurejea kwao.

Salum Abdallah alihamia Tabora mwaka wa 1947 baada ya “locoshed” kama karakana ya treni ilivyokuwa ikijulikana ilipohamishiwa Tabora na mwaka huo huo Salum Abdallah aliongoza mgomo mkubwa wa wafanyakazi wa relwe. Salum Abdallah aliishi Tabora hadi Mungu alipomuhitimisha mwaka 1974 na katika umri wake alifanya mengi katika siasa. Akiwa mwanachama wa African Association kutoka Dar es Salaam aliendeleza harakati pale Tabora na mwezi June 1954 yeye alikuwa mmojawapo wa wanachama wa TAA waliokutana kwa siri Town School kufanya mipango ya kumleta katibu wa TAA Tabora Germano Pacha kuja Dar es Salaam kuasisi TANU tarehe 7 Julai 1954. Salum Abdallah alikuwa mtu wa ari na akijiweza sana. Nyumba yake pale Isevya, Kanoni Street alipokuwa akiishi inasemakana ndiyo ilikuwa moja ya nyumba za mwanzo kupata maji ya bomba na umeme na kuwa na simu.

Salum Abdallah katika mkutano ule alitoa mchango wa shilingi ishirini kumsafirisha Pacha kuja Dar es Salaam. Wakati ule hizo zilikuwa fedha nyingi. 

Mwenyewe akisema kwa masikitiko kuwa alikuwa mtu wa mwanzo kumuunga mkono Nyerere katika kupigania uhuru. Mwaka 1955 Salum Abdallah alichaguliwa kama mwenyekiti muasisi  wa Tanganyika RailwayAfrican Union (TRAU) chama cha wafanyakazi wa Reli kilichokuwa na nguvu sana wakati wa kupigania uhuru na kikitoa mchango mkubwa kwa TANU. Katibu wa TRAU alikuwa Chistopher Kassanga Tumbo. Mwaka 1960 TRAU chini ya uongozi huu iliitisha mgomo uliodumu siku 82. Kwa miezi takriban miezi mitatu si treni, meli na mabasi ya relwe yalitembea. Inasemekana hapajatokea mgomo ambao ulitayarishwa kwa ufundi na ustadi kama mgomo wa relwe wa mwaka 1960. Mwishowe  serikali ya kikoloni ilisalimu amri na wafanyakazi wa relwe wakasitisha mgomo na kurudi kazini madai yao yote yakiwa yamekubaliwa. Mgomo huu miezi michache kabla ya Tanganyika kuwa huru ulimtisha sana Nyerere kwani alitambua kuwa kulikuwa na uongozi wa vyama vya wafanyakazi uliokuwa na nguvu sana na aliogopa baada Tanganyika kuwa huru vyama hivi chini ya viongozi kama hawa vitampa shida katika utawala wake. Katika mambo kama haya kunakuwa na mikasa mingi.

Salum Abdallah alikuwa na binti yake ambae kijana mmoja katika relwe alimpenda na akapeleka posa kwake kwa nia ya kutaka kufunga ndoa. Bahati mbaya kabla Salum Abdallah hajajibu posa ile mgomo ukawa umetokea. Sasa Yule kijana kwa bahati mbaya hakugoma kwa hiyo akawa katika kundi lililojulikana kama vibaraka. Salum Abdallah alihamaki sana kuwa yule kijana ambae alitegemea atajakuwa mkwe wake kaisaliti TRAU. Salum Abdallah akamwagiza mshenga wa yule kijana aje achuke majibu ya posa yake. Mshenga hakujua nini kinamsubiri. Siku ya siku ilipofika akajikusanya yeye na wenzake kwenda kupokea jibu la posa yao wakiwa na uhakika kuwa jibu litakuwa zuri na kitakachobaki ni kupanga siku ya harusi. Salum Abdallah alitoa kiti chake cha uvivu akakiweka sawasawa na mlango mkubwa wa nyumba yake anasubiri ujumbe ufike. Toka mbali Salum Abdallah anamuona mshenga na wapambe wake wale wanakuja na kanzu zao na kashda na ndani ya ujumbe kuna masheikh wawili watatu wa kuheshimika. Walitegemea chai nzito kwani Salum Abdallah hakuwa mtu mdogo katika jamii. Naam, hapakuwa chai wala salaam kama ilivyo kawaida wala Salum Abdallah hakumpa nafasi mchenga kusema chochote. Alinyanyuka na posa ya yule kijana akawatupia miguuni waiokote. Akawaambia, “Katafuteni mke kwa vibaraka wenzenu, nyumba yangu haingii kibaraka.” 

Huyo ndiye Salum Abdallah Muyiki Samitungo Mwekapopo. Mungu alimjalia tambo kasimama kama futi sita hivi. Akikuangalia tu unaondoka hata kabla hajakugusa. Mwezi wa Ramadhani wapiga ngoma ya daku watazunguka kote kisha watafika nyumbani kwake. Mwenyewe anakuwa kaka barazani anawasubiri. Wakishafika pale wanazima ngoma kama kuashiria kuwa sasa wanaingia katika “track” nyingie na hapo lile goma kubwa sondo litaanza kurindima kumwimbia nyimbo yake ya kumsifia ikiitwa “Ndege Mwema.”  Salum Abdallah atasikiza kisha atanyanyuka pale alipokaa atawaendea na kuwatunza fedha za kutosha hasa. Hapo watageuka na kuondoka huku “Ndege Mwema” ikirindima lakini kwa mpigo mwingine. Waswahili wana msemo, “Chini kunakwenda watu.” Yalipotokea maasi ya Tanganyika Rifles (TR) tarehe 20 Januari 1964, Salum Abdallah alikamatwa na kutupwa kuzuizini pamoja na viongozi wengi wa vyama vya wafanyakazi pamoja na masheikh. Sababu zilizotolewa ni kuwa kulikuwa na njama za kupindua serikali ya Nyerere na viongozi hao pamoja na masheikh walihusika katika njama hizo. Shutuma nyingine hasa kwa masheikh ilikuwa masheikh walikuwa “wanachanganya dini na siasa.” Haya yakitanguliwa na migongano mwaka 1963 migongano ambayo ilisababisha sintofamu kubwa kati ya Waislam na serikali ya Nyerere. Katika waazuoni maarufu waliokumbwa na hali hii alikuwa Shariff Hussein Badawy na mdogo wake Mwinyibaba. Hawa walikuwa walimu Masjid Badawy Kisutu karibu na Soko Mjinga. Msikiti huu sasa unaitwa Rawdha. Hawa walifukuzwa nchini na kurejeshwa kwao 

Mombasa. Ilikuwa katika utawala wa Ali Hassan Mwinyi ndipo waliporuhusiwa kurudi tena Tanzania. Shariff Hussein wakati ule miaka 1960 alikuwa kijana na akicheza mpira club ya Cosmopolitan. Matatizo haya yakatambaa hadi kufika mwaka 1968 na Sheikh Hassan bin Ameir aliyekuwa Mufti wa Tanganyika na Zanzibar nae akakamatwa na kurejeshwa Zanzibar na akapigwa marufuku asifike Tanzania Bara.

Salum Abdallah alipotoka kizuzini jela ya Uyui, si tu aliichukia TANU chama alichokipenda bali alimchukia hata Nyerere na hakujihushisha tena na siasa na alitumia muda wake mwingi katika ukulima wa tumbuku Urambo na alifanikiwa sana. Katika mazishi yake TANU ilisoma taazia na walimsifu sana kuwa Salum Abdallah akijulikana zaidi kwa jina la Baba Popo alikuwa mzalendo wa kweli na aliupigania uhuru wa Tanganyika kwa dhati. Haya ndiyo katika maajabu ya siasa. Kabla hajafa Salum Abdallah akitembea na shutuma kuwa yeye na wenzake walipanga njama za kupindua serikali ingawa kesi ile ya maasi ya jeshi ilipokwenda mahakamani Salum Abdallah na viongozi wenzake wa vyama vya wafanyakazi na msheikh hawakuunganishwa katika mashtaka ya uhaini.

Nyumba ya mwisho Kipata na New Street ilikuwa nyumba ya Bi. Mluguru bint Mussa mama yake Abdulwahid, Ally na Abbas Sykes. Ilipokuwa nyumba hii leo ndipo lilipo jengo la Ushirika. Nyumba hii wakati Tanganyika inaanza kuvitia nguvu vyama vya ushirika walitaka kujenga jumba la ushirika Dar es Salaam. Inasemekana Nyerere alituma salaam maalum kwa Bi Mluguru kupitia kwa mwanae Abbas aiuzie serikali nyumba yake ilipate kiwanja cha kujenga jumba lile la ushirika na hicho ndicho kilichofanyika. Bi Mluguru aliiuzia serikali nyumba yake. Huyu Bi Mkubwa ni kati ya wanawake watu wazima wa mwanzo kumkaribisha Nyerere katika nyumba zao. Kuna kisa mashuhuri kati ya Nyerere na Bi Mluguru. Baada ya uhuru kupatikana mengi yakapita na waliokuwa karibu na Nyerere ghafla wakajikuta wako nje ya ulingo lakini maisha hayakusimama yaliendelea kama ilivyo ada.

Siku moja Nyerere akiwa ndani ya msafara wake wa mapikipiki akienda Gerezani kufungua mradi wa viwanda vidogo vidogo, msafawa wake uliingia Mtaa wa Sikukuu ukawa unaelekea mitaa ya Kiungani. Nyerere akiwa ndani ya benzi lake alikuwa akitupa macho huku na huku akiangalia mitaa yake aliyokuwa akiikanyanga kwa miguu enzi za kudai uhuru. Bila shaka msafara ulipopita Kipata na Sikukuu Nyerere aliiangalia nyumba ya Mzee Mtamila, msafara ulipoingia Sikukuu na na Kirk kuna shaka alinyoosha shingo yake kuangalia nyumba aliyoijua sana, nyumbani kwa Abdulwahid Sykes na mama yake Bi Mluguru. Hapa jicho la Nyerere likagongana na sura ya Bi Mluguru aliyekuwa amejipanga mstari pamoja na wananchi wengine kuangalia msafara wa Nyerere. Alipotambua kuwa yule mama aliyesimama alikuwa Bi Mluguru, Nyerere aliamua gari yake isimame na kwa ghafla dereva wake alisimamisha gari. Nyerere alitoka nje ya gari akamwendea Bi Mluguru kumwamkia. Mapikipiki yalisimama madereva wamepigwa na butwaa. 

Wanaangalia nyuma wanamuona Nyerere anazungumza na mama mmoja mtu mzima. Haraka walinzi wakawa wamemzunguka Nyerere na Bi Mluguru. 

Kwa hakika kitendo kile kilikuwa cha kushangaza. Nyerere alipoondoka na msafara wake nyuma aliacha gumzo kubwa. Ilikuwa miaka michache baada ya kifo cha Abdulwahid. Walioijua historia ya Nyerere na marehemu Abdulwahid  Sykes kitendo kile cha kiungwana cha Nyerere hakikuwashangaza. 

Tabu walipata wale waliokuwa hawaijui vyema historia ya Nyerere alipofika Dar es Salaam kutokea Musoma mwaka wa 1952 na kupokelewa na Abdulwahid Sykes akiwa Rais wa TAA.

Katika nyumba ile ya Bi Mluguru ndiyo tumefika mwisho wa Kipata Street. Sasa tuingie mtaa unaofuatia, Somali Street. Nyumba ya baba yake Zuberi Mtemvu, Mzee Mwinshehe Mmanga Mtemvu nyumba ilikuwa inapeana mgongo na nyumba ya Kleist Sykes. Zuberi Mtemvu alikuwa mmoja wa vijana wa mwanzo kuiunga mkono TANU hata kabla haijajulikana sana. Wakati Abdulwahid na Ally Sykes, Dossa Aziz, John Rupia na Nyerere wanafanya mipango ya kuibadili TAA kuwa chama cha siasa kamili, Ally alimnong’oneza Mtemvu kuhusu jambo hilo. Hapo hapo Mtemvu alimwambia Ally kuwa anaunga mkono jambo hilo. Mtemvu akamfuata Ally Mwinyi Tambwe na kufahamisha kuhusu TANU. Ally Sykes hadi leo katika nyaraka zake anazozithamini sana ni “note” aliyoandikiwa kwa penseli na Mtemvu akimfahamisha kuhusu kumpata Ally Mwinyi Tambwe kama mmoja wa watu wanaounga mkono TANU. Mara tu baada ya TANU kuundwa Mtemvu na Nyerere walikwenda Morogoro kwa Mzee Mwinshehe Mmanga Mtemvu baba yake Zuberi Mtemvu awasaidie kupata wanachama wa TANU.

Haukupita muda Nyerere akamshawishi Mtemvu aache kazi Welfare Department ajiunge na TANU kama secretary general. Hivi ndivyo Mtemvu akaja kuwa Secretary General wa kwanza wa TANU. Ugomzi wa Mtemvu na Nyerere ulisababishwa na uchaguzi mkuu wa kwanza mwaka 1958 uliokuja kujulikana kama Uchaguzi wa Kura Tatu. Mtemvu alikuwa na msimamo mkali akiamini Tangayika ilikuwa ya Waafrika na mataifa mengine hayakuwa na haki ya kudai utawala. Hakika uchaguzi huu ulitishia uhai wa TANU kwa kuwa Waingereza waliweka masharti ya kibaguzi ili Mwafrika aweze kuwa na uhalaili wa kupiga au kupigiwa kura. Hapa si mahali pake kueleza mkasa huu lakini itoshe tu kuwa baadhi ya viongozi katika TANU kama Said Chamwenyewe, Mashado Plantan, Saleh Muhsin Mende na wanachama wengine ingawa hawakuwa wengi  walichukizwa na uamuzi wa TANU kukubali kuingia katika uchaguzi ule na walijitoa TANU na kuanzisha chama kilichojulikana kama Congress kikiongozwa na Zuberi Mtemvu. Wanachama wa Congress walikuwa wakikiita chama chao “Congress mwamba usiovunjika.” Makao Makuu ya Congress yalikuwa Nyamwezi Street kona na Faru. Nyumba hii ya ghorofa moja baadae ilikujanunuliwa na mmoja wa wakongwe wa TANU Mzee Marsha Bilal. Mzee Marsha ni katika wanachama waliohudhuria mkutano wa kwanza wa TANU Arnatuoglo Hall mkutano ambao haukuzidi takriban watu ishirini, wengine walikuwa, Rajab Diwani, Ali Rashid Meli, Mashado Plantan na wengineo. Mkutano huu uliripotiwa katika gazeti lililokuwa likihaririwa na ndiye alikuwa mwenye mali ya wa gazeti hilo, Mashado Plantan.

Ukitoka nyumba ile kabla hujafika Livingstone Street unakuta nyumba aliyokuwa akiishi Mwalimu Bakari. Wengine walikuwa wakipenda kumwita Mwalimu Bakari Setihabari. Nadhani hii “Sethikhabari” ilikuwa kama sifa ikimaanisha mjuzi na mtu wa kujua mambo mengi. Huyu hakuwa mwanasiasa bali alikuwa bingwa kwa majini. Tulivyokuwa watoto tulikuwa tukisikia wakubwa wakisema kuwa Mwalimu Bakari hana mke lakini majini ndiyo wanaomsafishia nyumba yake na kuwa safi kabisa na kumfulia nguo zake. Kwa hakika Mwalimu Bakari alikuwa nadhifu sana. Akipenda kuvaa kanzu nyeupe pyee, koti na kilemba. Watu wakisema watumishi wake walikuwa maruhani. Mwalimu Bakari alikuwa maarufu si Gerezani tu bali Kariakoo nzima kwani alikuwa bingwa wa kupunga pepo. Siku ya Jumapili ilikuwa ndiyo siku maalum kwa kazi hiyo. Wagonjwa waliokuwa wameathriwa na majini wakupungwa kwa kusomewa na kulishwa chano. Chano ni mfano wa sinia lakini hutengenezwa kwa mbao.

Basi hiki chano hujazwa vyakula vya kila aina kama hulua, tende, sukari mawe nk. Kisomo mgonjwa na mara zote huwa wanawake huwekwa kwenye kiti na kisomo huanza na wakati mwingine nyimbo zinaimbwa. Taratibu utaona mgonjwa ambae huwa akafunikwa shuka nyeupe gubigubi huanza kucheza na hiyo huwa ni ishara kuwa jini anapanda na akijaa kichwani Mwalimu Bakari alikuwa akimsemesha na kupitia yule mgonjwa jini anazungumza na kusema anachokitaka ili amwachie mgonjwa na maradhi yamtoke. Wakati mwingine jinni hudai farasi. Kwa lugha zile za kijini hiyo humaanisha kuwa anataka achinjiwe mbuzi au kuku. Hilo hufanyika na ile damu hunywewa na yule mgonjwa. Wakati mwingine shughuli huwa kali maana jinni wa mgonjwa akipanda na wale wanawake waliokuja kushuhudia na wao hupandisha maruhani wao. Hapo kazi huwa pevu. Kama vile namuona Mwalimu Bakari, kanzu kaikunja kaifunga kiunoni ubani unawaka kwenye kitezo anahangaika huku na huku huku akisoma na haipiti muda wale wanawake wote hutulia.

Kwa hakika baada ya tiba hii mgonjwa anarudia hali yake ya awali na kuzungumza kama anavyozungumza katika hali yake ya kawaida. Vitu vilivyobakishwa kama tende, sukari mawe, haluwa hupewa watoto waliokuja kuhudhuria shughuli ile. Watoto tulipenda kuhudhuria shughuli hizi kwa kufata vile vitamu na baada ya muda tukawa tunazijua hata zile nyimbo za pungo. Lakini ibra moja ni kuwa ndani ya nafsi zetu tulikuwa tunahisi kuwa lile halikuwa jambo la mchezo, lilikuwa jambo la kutisha. Hatukuwa tukiziimba nyimbo zile katika michezo yetu ya kitoto. Haya ndiyo yalikuwa maisha ya watu wa Dar es Salaam katika miaka ile ya 1950. Miaka mingi baada ya mwandishi kupata makamo na kuijua dunia hakupata tabu kuainisha yale aliyoyaona utotoni yakifanywa na Mwalimu Bakari na sherehe za vodoo ambazo ni maarufu katika visiwa vya Haiti na sehemu nyingi za Caribbean. 

Tofauti ni kuwa wenzetu bado wanaendelea na mambo hayo wakati huku kwetu haya mambo yamefifia sana. Kwa kumaliza nukta hii ningependa kueleza kuwa hata katika Baraza la Wazee wa TANU walikuwapo “mafundi” na leo ukitazama katika picha za zamani za harakati za uhuru wanaonekana karibu ya Mwalimu Nyerere wamevaa kanzu, koti na kofia. Mmoja katika hawa alikuwa Sheikh Issa Nassir wa Bagamoyo. Kuna picha ilipigwa nje ya Ukumbi wa Karimjee inamwonyesha Mwalimu Nyerere kabebwa huku ameshika bango “Uhuru 1961” pembeni yake yuko Rajab Diwani. 

Ukiangalia kwa pembeni utamwona Sheikh Issa Nassir. Inasikitisha kuwa hadi hii leo serikali haijafanya juhudi yoyote ya kuandika historia ya uhuru wa Tanganyika na kwa ajili hii historia hiyo sasa imepotea na haifahamiki. Wasomi na wanafunzi wa historia ya Tanganyika wawatafiti wazalendo hawa na kazi zao ndani ya TANU.

Ukivuka Livingstone ndiyo unafika sasa katika nyumba ya Bi Mluguru bint Mussa mama yake Abdulwahid Sykes. Kuna kisa kimoja, kilitokea hapa wakati wa kudai uhuru, viko vingi lakini kwa ajili ya muda ntaeleza hiki kimoja. Siku moja Nyerere alikuwa pale Kirk Street pamoja na Abdulwahid Sykes na Mama Maria na mama yake Nyerere Bi Mugaya pia alikuwapo. Ghafla Nyerere alipindukwa na tumbo na akawa katika maumivi makali sana. Hali ilipozidi kuwa mbaya, Mama Maria akamwita pembeni Bi Mwamvua biti Marsha maarufu akijulikana kama Mama Daisy, mke wa Abdulwahid na kumwambia kuwa mama yake Nyerere Bi Mugaya ana wasiwasi kuwa mwanae anakufa kapewa sumu. Mama Maria hofu ilikuwa imempata na akawa na wahka mkubwa. Mama Mugaya akamnong’oneza Bi Mluguru kuwa ana wasiwasi kuwa aliyempa sumu mwanae si mtu wa mbali. Nyerere hakuwa amelishwa sumu.

Ukitoka nyumba ya Bi Mlu guru sasa kabla hujakatiza Sikukuu Street mkono wa kulia kulikuwa na kinyozi aliyekuwa maarufu akiwanyoa watu wote wa Gerezani na kwengineko akijulikana kwa jina moja tu la Muingereza. Muingereza alikuwa akinyoa chini ya mti na umuhimu wa mahali pale ilikuwa ni barza wakikutana watu kwa mazungumzo hasa nyakati za alasiri. Hapa katika miaka ya 1950 mazungumzo yalikuwa siasa tu. Leo Gavana Twining kasema hili, leo Nyerere kajibu vile, Bi Titi kawashambulia wakoloni, Mtemvu kafanya hiki na habari zote zilikuwa zikifika pale na kuwekwa uwanjani kwa mjadala. Wakati gumzo likiendelea sauti ya mkasi wa Muingereza ulikuwa ikisikika ikila nywele katika kichwa kat, kat, kat... na yeye mwenyewe Muingereza alikuwa mtu wa vichekesho sana hakuwa nyuma katika kutupa neno hapa na pale kama vile, “Sikiiza bwana huyu Twining, Nyerere  kesha mtafutia mbeleko yake, atabebwa tu hana ujanja.” Hapo pembeni anaweza kuwa amekaa Abdulwahid, Dossa na jamaa wengine tena wamekalia gogo (maana kwa Mwingereza kulikuwa hakuna viti) lakini wote wakiunganishwa na mapenzi yao kwa TANU. Baadae ilipokuja Congress kama chama cha upinzani wanachama wa Congress hawakukosa pale na barza sasa ikiwa imestawi hasa. Mijadala kati ya TANU na Congress kwa kawaida ilikuwa mikali hata kushinda ya Sunderland na Yanga.

Mazungumzo yatabadilika siku Sunderland wako uwanjani Ilala Stadium wakicheza na Yanga. Hapo tena siasa inawekwa pembeni mazungumzo yanahamia kwenye mpira na washabiki wa timu zote walikuwa wanabaraza wa Kinyozi Muingereza. Wakati ule Yanga walikuwa na mchezaji wao maarufu bingwa wa kupiga kona Hamisi Mtoto tena yeye mwenyewe alikuwa mkazi wa Gerezani, Mtaa wa Somali Street kona na Sikukuu. Sunderland wakijuvunia Harold Mgone walompachika jina “Wamisalaba,” Mashaka Abdallah maarufu kwa jina la “Mashaka Prince,” Salum Kheri Kilanga, Salum Ali maarufu kwa jina la “Jini” na wengineo, (kisa cha Salum Ali kuitwa jinni ni kuwa alikuwa akitumia mguu mmoja tu katika uchezaji wake. Salum Ali alicheza mpira hadi katika miaka ya 1960 katikati), huyu Kilanga alikuwa Yanga kisha akahamia Sunderland. Wakati huo huo Mambo Mzinga aliyekuwa Yanga nae akatoka akaenda Sunderland. Mambo Mzinga alikuwa mwalimu wa madrasa iliyoanzishwa na baba yake Sheikh Mzinga. Watoto wengi wa Dar es Salaam wamesoma chuo hiki ambacho kipo hadi leo Mtaa wa Mafia kona na Chura. Yanga walikuwa na wachezaji wengine wakali kama Stumai Mzee, Juma Mbimbi, Hamisi Fotini, Badr Malande, Mwenda Mushi na wengineo. Baadhi ya wachezaji hawa ndiyo walichukua kombe la Gossage mwaka 1949.

Ukitoka kwa Mwingereza sasa unakwenda Kirk Street kona na Nyamwezi mkono wa kushoto iilikuwa nyumba ya Saleh Muhsin Mende mmoja wa wanachama wa TANU. Nyumba hii ilikuwa ya ghorofa moja na moja ya yumba nzuri sana kwa wakati ule. Saleh Muhsin Mende alikuwa mchanganyiko wa Muarabu na Mwafrika. Ukoo wao walikuwa na hodhi kubwa sana Kurasini. Saleh Muhsin Mende alitoka TANU pamoja na Zuberi Mtemvu kuunda Congress. Baada ya uchaguzi wa 1963 ambao Congress ilishindwa vibaya Mtemvu aliamua kuivunja Congress. Saleh Muhsin Mende alionyesha hisia zake aliuchukulia vipi uamuzi ule wa Mtemvu miaka takriban arobaini baadae na ilikuwa kwenye harusi ya mjukuu wake. Mtoto wa Mtemvu alimposa mjuu kwa Saleh Muhsin Mende. Siku ya maulid ya harusi nyumbani kwake pale Kirk Street (sasa Lindi), wazee wengi wa Gerezani walikuwa wamejumuika pale wakikumbushana mambo ya zamani. Saleh Muhsin akasimama huku anacheka akasema, “Mimi nilimuasa President wangu wa Congress, Zuberi, bwana kwa hisani yako usivunje chama nimemsihi lakini hakutaka kunisikiliza. Congress ikavunjika nasi tukatawanyika. Leo Zuberi huyu karudi miguuni kwangu.” Pakawa na vicheko na Mtemvu mwenyewe akawa anacheka. Baada ya kuvunjika kwa Congress wengi wanachama wake walirejea TANU lakini ule moto wa hamasa waliokuwa nao katika TANU ya miaka ya 1950 haukuwepo tena.

Ukivuka Nyamwezi Street sasa mkono huo huo wa kushoto unafika nyumbani kwa Mashado Ramadhani Plantan, mwanachama shupavu wa African Association, TAA, TANU na All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT). Mashado Plantan alizaliwa Mozambique mwaka 1900 na alikuja Tanganyika mkwaka wa 1905 akiwa mtoto mdogo wa miaka mitano. Mashado Plantan ni miongoni mwa wanachamwa mwanzo wa TANU na Mwafrika wa pili katika Tanganyika kuwa na gazeti lake mwenye, Zuhra. Mwafrika wa kwanza kuwa na gazeti alikuwa Erika Fiah, Mwafrika kutoka Uganda aliyelowea Tanganyika. Gazeti lake likiitwa “Kwetu” Mashado Plantan ndiyo alikuwa mzalendo wa kwanza kuifanyia propaganda TANU na kumjulisha Nyerere kwa wananchi wa Tanganyika kupitia gazeti lake la Zuhra. Mashado Plantan, Kleist Sykes na Mdachi Sharifu ni miongoni mwa watu waliohudhuria sherehe ya ufunguzi wa jengo la African Association, New Street mwaka wa 1933 jengo ambalo lilifunguliwa na Gavana Donald Cameroon. Baada ya Uchaguzi wa Kura Tatu na ugomvi uliotokea baina ya Mwenyekti wa Baraza la wazee wa TANU Dar es Salaam na Julius Nyerere mwaka wa 1958  Mashado alitoka TANU yeye na wanachachama wengine kuunda AMNUT na nyumba yake ikawa ndiyo ofisi ya kwanza ya chama hicho. Mashado aliondoka duniani akiwa na kinyongo na TANU jinsi ilivyovunja ndoto za wengi walioweka matumaini makubwa katika uhuru wa Tanganyika. Alimaliza siku zake akitumia muda wake mwingi katika msikiti wa Sheikh Juma Tego Mtaa wa Lindi.

Sasa tuingie mitaa ya kukatisha iliyoko Gerezani. Mtaa wa Mbaruku ndiko ilipokuwa nyumba ya Dossa Aziz mtoto mkubwa wa Aziz Ali mmoja wa Waafrika tajiri siku zile. Dossa alikuwa mfadhili mkubwa wa TANU. Dossa alitoa gari yake kuipa TANU na hii ikajakuwa gari ya mwanzo kumilikiwa na TANU katika shughuli zake za kuikomboa Tanganyika kutoka makucha ya Waingereza. Nyumbani kwa Dossa ndiko palipokuwa na Baraza ya TAA mahali ambapo wanasiasa Waafrika walikutana kila Jumapili kupanga mikakati ya kumng’oa Mwingereza katika ardhi ya Tanganyika. Nyerere alikuwa akija kila Jumapili pale nyumbani kwa Dossa na kukutana na viongozi wa TAA. Baraza hili lilikuwa aidha Mbaruku kwa Dossa au wakati mwngine Stanley Street kona na Sikukuu nyumbani kwa Abdulwahid Sykes. Dossa, Abdulwahid na Ally Sykes, John Rupia na Julius Nyerere ndiyo walikuwa katika kamati ya ndani katika kuisukuma TAA kuwa chama kamili cha siasa na ilifanya kazi hii kwa siri sana kati ya mwaka 1953 hadi 1954 walipounda TANU tarehe 7 Julai.

Aziz Ally baba yake Dossa alikuwa Mdigo kutoka Mombasa na alikuja Dar es Salaam baada ya Vita Kuu ya Kwanza akafanya kazi ya ujenzi wa majumba na akatajirika sana. Dossa alikuwa Mwafrika wa kwanza kununua gari na alikuwa akiendeshwa na dereva. Aziz Ally nyumba yake ya vigae na vioo hadi leo ipo pale Mtoni kwa Aziz Ally ambako alikuwa na hodhi kubwa ya ardhi. Aziz Ally alijenga nyumba nyingi za Waafrika kama mkandarasi na vilevile alijenga miskiti mingi kama sadaka yake kwa Mungu. Wakati Dar es Salaam hakuna umeme yeye ndiye aliyechukua jukumu la kupeleka karabai katika misikiti yote ya pale mjini. Hamza Aziz wakati ule kijana mdogo ndiyo aliepewa kazi ile ya kutia taa zile mafuta, kuzisafisha na kuzipeleka kila msikiti kabla ya Sala ya Maghrib na kuzichukua kuzirudisha nyumbani kwao Mbaruku baada ya Sala ya Isha ili ziwe tayari kutumika siku ya pili. Aziz Ali alipokufa mwaka wa 1951 gazeti la Tanganyika Standard liliandika kifo chake kwa kichwa hiki cha habari kilichosema, “Mjenzi wa Misikiti Amekufa.”

Aziz Ally aliwaachia watoto wake nyumba nyingi mjini Dar es Salaam lakini katika mali za Aziz Ally ambazo zilisaidia harakati za uhuru moja kwa moja ilikuwa ni malori saba ya kubeba mchanga na kokoto ambayo yalikuwa chini ya Dossa Aziz. Hii ilikuwa mali nyingi sana na Dossa mkono wake ulikuwa wazi si kwa TANU tu bali hata kwa Nyerere mwenyewe. Lakini juu ya ukarimu wake huu na mchango wake mkubwa katika harakati za kudai uhuru hakuna aliyethamini yote aliyomfanyia Nyerere, TANU na Tanganyika. Dossa amekufa masikini kijijini Mlandizi mwaka 1998. Ingawa mazishi yake yalihuidhuriwa na wanachma wengi wa iliyokuwa TANU na ingawa CCM ilijiweka mbele katika mazishi yake, tanzia iliyosomwa pale haikumueleza Dossa kama alivyokuwa. Sababu kubwa ni kuwa pale mazikoni hakuna aliyemjua vyema Dossa. Labda kama Nyerere angekuwapo mazikoni angeweza kumueleza Dossa na kumpa hadhi aliyostahili, lakini Nyerere hakuhudhuria mazishi ya Dossa. Dossa alifikia hali ya kuwa alishindwa kwenda kwenye mkutano wa Kizota mwaka 1987 kwa kuwa hakuwa na nguo za kuvaa na kama si rafiki yake wa utotoni Abbas Sykes kumnunulia nguo na viatu na kumshawishi wafuatane pamoja Dodoma, Dossa asingelihudhuria mkutano ule.

Wakati wa enzi yake baada ya mkutano wa TANU pale Mnazi Mmoja ambako Nyerere alihutubia, kundi la wana TANU, Nyerere, Abdulwahid, Ally na jamaa wengine walikuwa wanakutana Princess hotel kwa tafrija ndogo ya kupongezana na kufanya tathmini ya mkutano. Siku zote na kwa miaka yote hadi uhuru ulipopatikana, Dossa ndiyo alikuwa akilipa gharama zote kutoka mfukoni kwake. Tusogee kidogo Mbaruku Street na Somali Kipande, hapa ndipo ilipokuwa nyumba nyingine ya Aziz Ally ambayo alikuwa akikaa Biti Ali mmoja wa wake wengi wa Aziz Ali. Nyumba hii ni moja ya nyumba ambazo Nyerere akifuatana na Dossa akiingia na kukarimiwa na mama huyu. Biti Ali yu hai na anaishi Ilala. Mama huyu ni hazina ya historia ya TANU na siku za mwanzo za kudai uhuru. Kwa kumaliza hebu tufike Livingstone Street kona na Kipata unaelekea Kiungani mkono wa kushoto kulikuwa na nyumba ambamo kulikuwa studio ya Mzee Shebe. Mzee Shebe ndiye alikuwa mpiga picha wa mwanzo wa TANU na Nyerere na ameacha hazina kubwa ya historia ya TANU na Nyerere katika picha. Ukitaka kuijua historia ya TANU na matokeo yote kuanzia 1954 hadi uhuru ulipopatikana nwaka 1961 pitia picha za Mzee Shebe ambazo hivi sasa hazina hii imehifadhiwa na watoto wake mjini Dar es Salaam.

Mwandishi  Akiwa na Mwaka Mmoja Au Miwili 
Picha Aliyopigwa na Mzee Shebe 1952/53 
Kwenye Studio Yake Mtaa wa Livingstone na Kipata

0 comments:

Post a Comment

99Graphix

99Graphix
99Graphix
Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!